Polisi waliokamatwa kufuatia kutoroka kwa mahabusu Gigiri nje kwa dhamana
MAAFISA watano wa polisi waliokamatwa kufuatia kutoroka kwa mahabusu 13 kutoka kituo cha polisi cha Gigiri, miongoni mwao Collins Jumaisi, mshukiwa mkuu wa mauaji ya wanawake 42 ambao miili yao ilipatikana kwenye timbo jijini Nairobi, Alhamisi, Agosti 22, 2024 waliachiliwa kwa dhamana ya Sh200, 000.
Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Milimani Martha Nanzushi alikataa ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) la kuwazuilia kwa siku 14 na badala yake akaawaagiza wawe wakiripoti kwa afisi za DCI mara mbili kwa wiki hadi uchunguzi utakapokamilika.
Bi Nanzushi aliwaonya watano hao dhidi ya kuingilia na kuvuruga uchunguzi.
Akiwaachilia kwa dhamana Koplo Ronald Babo, na makonstebo Evans Kipkirui, Zachary Nyabuto, Millicent Achieng na Gerald Mutuku, hakimu alisema upande wa mashtaka haukutoa sababu za kutosha kuridhisha korti kwa nini wanafaa kuzuiliwa.
“Baada ya kuchanganua ombi la polisi la kuwazuilia washukiwa kwa siku 14 sioni sababu yenye nguvu kukubali ombi hilo. Ninakataa ombi hilo na kuwaachilia watuhumiwa kwa dhamana ya Sh200, 000,” akasema hakimu.
Maafisa hao walikuwa zamu usiku wakati mahabusu 13 akiwemo Jumaisi walipotoroka kutoka seli za polisi akisubiri kufunguliwa mashtaka ya mauaji.
Mahabusu wengine 12 walikuwa raia wa Ethiopia waliopatikana nchini kinyume cha sheria.