Askofu wa Amerika alalamikia mfumo wa haki nchini
ASKOFU anayehubiri nchini Amerika alieleza Mahakama ya Nairobi mnamo Jumanne Agosti 20, 2024 kwamba hawezi kujihusisha na ulaghai wowote kwa vile ameekeza zaidi ya Sh1 bilioni humu nchini.
Askofu David Nyamasyo Ndunda Kitonga aliyestawisha hoteli ya kifahari almaarufu Kitonga Resort iliyoko eneo la Mbiuni, Kangundo, Kaunti ya Machakos, alishangaa jinsi “anavyolaghaiwa kisha ashtakiwe kulaghai.”
Askofu Kitonga alilalamikia mfumo wa haki humu nchini.
Kupitia kwa wakili wake, Askofu Kitonga na mkewe Monica Ndunge Kitonga, walimweleza hakimu mkuu mahakama ya Milimani Susan Shitubi kwamba wameshangazwa na mfumo wa haki nchini.
Bi Shitubi alifahamishwa kuwa wawili hao walioshtakiwa kumlaghai Gabriel Njenjere Chokera bao za ujenzi (TNG) za thamani Sh15, 199 ,240 wameshangaa sababu ya kushtakiwa.
Mtu na mkewe hao walikana wakiwa na nia ya kulaghai walipokea bao za TNG kutoka kwa Gabriel Njenjere Chokera.
“Hii ni deni. Hatuelewi sababu ya kuburutwa na kufikishwa kortini ilhali pia tunamdai mlalamishi,” wawili hao walimweleza hakimu huku wakiomba waachiliwe kwa dhamana.
Wakili anayewawakilisha wawili hao alieleza Bi Shitubi, “Kitonga amewekeza humu nchini zaidi ya Sh1 bilioni. Atawezaje kushiriki ulaghai wa Sh15 milioni ilhali amewekeza mabilioni ya pesa katika mkahawa wa kifahari wa Kitonga Resort eneo la Mbiuni, Kangundo, Machakos?”
Kiongozi wa mashtaka Wanjiru Waweru hakupinga wakiachiliwa kwa dhamana.
Wakili wa mlalamishi (Njenjere) Henry Kurauka aliomba Kitonga na mkewe Ndunge washurutishwe kuweka pasipoti zao kortini kwa vile “wanaishi Amerika na wakirudi huenda wasirejee nchini kufanya kesi.”
Mahakama iliwaachilia wawili hao kwa dhamana ya pesa taslimu Sh500, 000.
Na wakati huo huo, Bi Shitubi aliwataka wawili hao waweke pasipoti zao kortini kama mojawapo ya sharti la dhamana.
Sasa itabidi wawili hao wakitaka kusafiri wapewe idhini na mahakama.
Kesi hiyo itatajwa baada ya wiki mbili, mhubiri huyo na mkewe wapewe mwelekeo jinsi kesi itakavyoendelea.