Sh4.2 bilioni za KAA’ zakunywa maji’ kufuatia dili kombo ya ujenzi wa lango JKIA
MAMLAKA ya Kusimamia Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) imepata hasara ya Sh 4.2 bilioni kwa mwaka uliotamatika Juni 2023 kufuatia ulipaji wa Sh5.4 bilioni kwa wanakandarasi wawili raia wa Uchina.
Malipo kwa wanakandarasi hao, yanafuatia masikizano ya pande hizo mbili kutatua mzozo uliokuwepo baina yao nje ya mahakama, kutokana na kufutwa kwa zabuni ya pamoja ya ujenzi wa lango la pili katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) miaka tisa iliyopita.
Hasara hiyo ni pigo kubwa kwa KAA, ambayo ilikuwa imetengeneza faida ya Sh 43.3 milioni katika mwaka wa kifedha uliopita.
Shirika hilo la serikali, lilikuwa limewapa wanakandarasi wawili wa Uchina- Anhui Civil Engineering Group (ACEG) na China Aero Technology Engineering International (Catic) zabuni ya kujenga lango la pili JKIA lakini ujenzi huo haukufanyika kama walivyoelewana.
“Katika mwaka huo, (KAA) ilifanya majadiliano na mwanakandarasi ACEG kuhusu kulipa Sh 17.6 bilioni,” KAA ilisema.
“Wahusika walikubali kulipa malipo yote na ya mwisho ya Sh614, 328, 659 na Sh4, 792, 805, 324.69 zingefutwa. Kufutwa huko kuliidhinishwa na Baraza la Mawaziri,”
Malipo ya hivi punde ya KAA, yanasukuma hesabu yote kwa mwanakandarasi huyo hadi Sh9.6 bilioni.
Mhasibu Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu hata hivyo ameuliza maswali kuhusu malipo hayo, akihoji kuwa KAA haikutoa ushahidi wa kuonyesha kuwa yaliidhinishwa na baraza la Mawaziri.
Bi Gathungu aliongeza kuwa stakabadhi za malipo ya mwisho hazikuwasilishwa kwa ukaguzi licha ya kwamba nakala za malipo ziliwasilishwa kwao na Mwanasheria wa Serikali.
Kenya ilikuwa imelipa Sh4.2 bilioni kwa ujenzi wa lango hilo, ambalo linajulikana kama Green Field Terminal, ambalo lingekuwa katika uwanja wa JKIA kati ya kilomita 0.75- 1.5 Mashariki mwa lango la Kwanza.
Lango hilo jipya lingehusisha sehemu ya pili ya ndege kukimbilia na lingegharimu Sh56 bilioni.
KAA, hata hivyo, ilifutilia mbali zabuni hiyo mnamo Machi 2016.
Wakichukizwa na hatua hiyo, wanakandarasi hao walitaka walipwe hasara walizozipata.
Wanakandarasi hao ambao wangefanya kazi kwa pamoja awali walidai Sh17.6 bilioni, lakini baadaye wakazipunguza hadi Sh9.6 bilioni.
Imetafsiriwa na Wycliffe Nyaberi