Habari za Kitaifa

Mgomo: Walimu wakaa ngumu shule zikifunguliwa Jumatatu


SEKTA ya elimu inakumbwa na hali tata shule zikifunguliwa kwa muhula wa tatu wiki ijayo.

Haya yanajiri huku mgomo wa walimu ukinukia katika kipindi muhimu cha mitihani.

Mgomo huo unaweza kuathiri kalenda ya elimu iwapo serikali haitafikia mwafaka na vyama vya walimu.

Mawaziri watatu wamejipata katika hali ngumu katika jitihada za kusimamisha mgomo ulioitishwa na walimu 406,635 kutokana na malalamishi kadhaa kwa Tume ya Huduma ya Walimu (TSC).

Ili kupata suluhu, macho yote yanaelekezwa kwa Waziri wa Fedha John Mbadi, Dkt Alfred Mutua (Waziri wa Leba na Ulinzi wa Jamii) na Bw Julius Mgosi Ogamba (Waziri wa Elimu).

Hii ni kufuatia agizo la Rais William Ruto kwamba wakutane na vyama vya wafanyakazi na kutatua masuala yaliyoibuliwa na walimu hao.

Mbadi awasha moto

Bw Mbadi amezidisha mzozo huo kwa kutangaza Alhamisi kuwa serikali haina pesa za kukidhi matakwa ya walimu.

Waziri huyo alifichua kuwa serikali ina uhaba wa fedha za kuajiri walimu 46,000 wa Sekondari Msingi kwa mikataba ya kudumu na pensheni.

Hii ni pamoja na kuajiri walimu wapya 20,000 kama vinavyotaka vyama vya wafanyakazi.

Kuna upungufu wa Sh 13 bilioni katika bajeti ya TSC.

‘Hakuna fedha zinazopatikana  labda tufanye marekebisho ya bajeti lakini kwa sasa hakuna nafasi,’ Bw Mbadi aliambia runinga ya Citizen Alhamisi usiku.

Chama cha Kitaifa cha Walimu nchini (KNUT) na Chama cha Walimu wa Walimu wa Shule za Upili na vyuo (KUPPET) vimewataka wanachama wake kuanza mgomo Jumatatu Agosti 26, 2024 shule zitakapofunguliwa kwa muhula wa tatu na wa mwisho mwaka huu.

Kufikia sasa, zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya shule kufunguliwa na mgomo huo ukinukia, Bw Ogamba hajafanya mkutano na vyama vya wafanyikazi na amekuwa akifanya shughuli zake zingine badala ya kuongoza mazungumzo na walimu.

Akiwa Mombasa, wakati wa Kongamano la Kimataifa la Wakuu wa Shule lililomalizika hivi karibuni, Waziri alitoa wito wa mashauriano ya washikadau ili kuepusha mgomo wa walimu unaokaribia akisema unaweza kuathiri kalenda ya elimu.