• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Alfred Mutua asema Kenya Kwanza nd’o mpango mzima

Alfred Mutua asema Kenya Kwanza nd’o mpango mzima

NA SAMMY WAWERU

GAVANA wa Machakos Alfred Mutua ametetea vikali hatua yake ya kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais Dkt William Ruto.

Dkt Mutua amekuwa mwanachama wa Azimio, muungano unaoongozwa na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, na mnamo Jumatatu alitangaza kuugura akajiunga na kambi ya Dkt Ruto.

Kiongozi huyo wa Maendeleo Chap Chap alisema chama chake kilichukua hatua kuondoka Azimio kwa kile alidai kama “kuchezewa karata kupitia mkataba wa makubaliano”.

Jumanne, kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, Mutua alisema uamuzi wake kujiunga na Kenya Kwanza ni kwa manufaa ya jamii ya Wakamba au Ukambani kwa ujumla.

Alisema kwa muda wa miaka 10 iliyopita, jamii hiyo imekuwa nje ya serikali kwa kile alidai kama kupotoshwa na kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, ambaye ana ushawishi mkubwa Ukambani.

“Jamii ya Ukambani haitakaa kwenye kijibaridi tena serikali ijayo. Kenya Kwanza ndiyo itaunda serikali, na naibu rais, Dkt William Ruto ameonyesha ukakamavu katika uongozi. Hatua yangu kujiunga na kambi yake ni manufaa kwa jamii ninayotoka,” Dkt Mutua akaelezea.

Gavana huyo amekuwa mkosoaji mkubwa wa Ruto, akimhusisha na sakata za ufisadi na ufujaji wa mali ya umma serikalini.

Mutua hata hivyo alipuuzilia mbali ‘mashambulizi’ hayo, akimmiminia naibu rais sifa na kumtaja kama kiongozi anayejali maslahi ya mwananchi wa kawaida.

Chini ya mfumo wa ‘bottom-up’, Ruto amekuwa akidai endapo atamrithi Rais Uhuru Kenyatta Agosti 9, atalenga kuboresha uchumi kutoka chini kuelekea chini.

“Watu huzaliwa wakiwa Wakristu na wanasilimu kujiunga na na dini ya Kiislamu, na wengine huzaliwa wakiwa Waislamu na wanajiunga na dini ya Kikristu,” Dkt Mutua akasema, akitetea uamuzi wake kujiunga na Kenya Kwanza.

  • Tags

You can share this post!

Mutua, Kingi watafuta hifadhi kwa Ruto, wadai kuumizwa...

Tuju apuuzilia mbali hatua ya Dkt Mutua kugura Azimio

T L