Habari za Kitaifa

Ruto sasa avumisha ‘handisheki’ yake na Raila kimataifa

Na TAIFA RIPOTA August 24th, 2024 1 min read

RAIS William Ruto anaonekana kufanikiwa kuzima kwa muda hasira za Gen-Z walioandamana majuzi, kwa kusuka uhusiano na chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM) ambao ameanza kuuvumisha kimataifa.

Maafisa wakuu wa serikali wanatangaza mpango huo mpya kwa washirika wa kigeni, wakiupamba kama demokrasia iliyokomaa na nchi ilivyo thabiti.

Japo wanasisitiza hakuna muungano wa vyama vyao, na hata ODM inayoongozwa na Raila Odinga inasisitiza kuwa haiko rasmi serikalini, ushirika wa Rais Ruto na Bw Odinga umevuka mipaka ya Kenya wakiuvumisha katika ngazi ya kimataifa.

Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi, katika taarifa, alifahamisha mabalozi wa nchi za kigeni jijini Nairobi kuhusu mpangilio mpya wa kiutawala katika Serikali Jumuishi.

‘Ili kufafanua wito wa rais, ningependa kusema tena kwamba huu ni wakati katika historia ya Kenya wa kutimiza matakwa ya watu wetu na kuweka kando maslahi ya vyama,’ akasema Bw Mudavadi.

Serikali Jumuishi, alisema, haibadilishi muundo uliopo, akisisitiza kuwa jukumu la Bunge bado lipo kumulika serikali.