Makala

IGAD yapendekeza sera ya watoto itakayodhibiti haki zao katika mataifa wanachama

Na WANGU KANURI August 28th, 2024 1 min read

JUMUIYA ya Mamlaka ya Kimataifa kuhusu Maendeleo (IGAD) imependekeza sera ya watoto ambayo itaongoza mataifa wanachama katika udhibitishaji wa haki za watoto.

Sera hiyo inakiri kuwa nchi tofauti zilizomo katika jumuiya ya IGAD zinakumbana na matatizo mbalimbali katika kudhibiti haki za watoto.

Changamoto hizo ni pamoja na vita, vurugu, umaskini, mazingira yasiyomkinga mtoto, kufukuzwa makwao, kutopata huduma za afya, na elimu.

Katika nchi zilizopo katika Jumuiya ya IGAD, watoto huratibu idadi kubwa.

Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Somalia, South Sudan, Sudan na Uganda, ndio nchi wanachama wa muungano huo.

Nchini Djibouti, kwa mfano watoto wanachangia idadi ya watu wote kwa asilimia 36, Eritrea 46, Ethiopia 46, Kenya 44, Somalia 54, Sudan Kusini 51, Sudan 47 na Uganda asilimia 52.

Changamoto ambazo watoto hawa hupitia katika juhudi za kuwakinga hutokana na watu binafsi, familia na hata jamii kwa ujumla.

Hata hivyo, sera hii ya watoto inanuia kuangazia elimu, lishe bora, usafi wa maji, mazingira na tabianchi, haki na usawa, amani pamoja na ulinzi wa watoto.

Ili watoto hao wanufaike, IGAD iliwahusisha katika mijadala ya kutengeneza sera hii ili maoni yao pia yakadiriwe.

Dkt Victoria Anib, Mkuu wa Maendeleo ya Jamii katika IGAD akihakikisha ahadi ya sera hiyo alisema, “Tunataka kuhakikisha kuwa sera hii inaangazia sera za kitaifa bila kuzipuuza bali kujazilia mapengo yaliyomo.”

Isitoshe, IGAD ilisema kuwa sera hii itasaidia nchi za jumuiya kuwa mstari wa mbele kupigania haki na ustawi wa watoto ili watoto wote watimize wanachonuia maishani.

[email protected]