Mama pima akwama kwa jombi eti amuoe

Na John Musyoki

Machakos Mjini

JAMAA anayeishi mjini hapa anajuta baada ya mama pima kukwamilia kwake baada ya kurushana roho.

Penyenye zinasema jamaa alimwalika mama huyo kwake naye hakusita kukubali mwaliko huo. Hata hivyo, baada ya wawili hao kuwa na wakati mzuri, jamaa alimtaka mamapima kurejea kwake lakini alikataa katakata kuondoka.

“Kwa nini unataka nirudi kwangu baada ya kukupa burudani ya aina yake. Kwani unanifukuza? Kwa taarifa yako mimi siendi mahali popote.Kuanzia sasa nitaendelea kuishi na wewe. Sitaki kuishi maisha ya upweke,” mamapima alimwambia jamaa.

Kulingana na penyenye jamaa alishangazwa na matamshi ya mama huyo.

“Ala, kwa nini unataka kuishi kwangu na hatukuwa na mpango huo? Hapana, haiwezekani ! Tulikubaliana kuwa na wakati wa kujivinjari tu halafu uondoke. Kwa nini sasa unabadilisha mawazo.

Mimi siwezi kukuoa kwa lazima. Kama unataka uwe mke wangu tutapanga baadaye lakini kwa sasa naomba uondoke,” jamaa alimwambia mama pima.

Hali ilizidi kuchacha mama alipolaumu jamaa kwa kutaka kumkataa.

“Kwa hivyo ulikuwa na haja ya kunitumia tu. Siondoki hapa na kuanzia sasa mimi ni mke wako. Nimechoka kuishi mtaani bila mume. Siendi mahali popote upende usipende,” mama pima alimwambia jamaa.

“Nyinyi wanaume furaha yenu ni kuona wanawake wakiishi peke yao. Kazi yenu ni kuwatumia na kuwatupa kama maganda ya muwa, samahani, ” mama aliwaka.

Jamaa aliaibika mbele ya majirani. Alipandwa na hasira za mkizi na kuondoka kuenda zake na kumwacha mamapima chumbani peke yake.

Hata hivyo haikujulikana kilichojiri baada ya kioja hicho.

 

Habari zinazohusiana na hii