Malalamishi yaibuka kutaka shughuli za serikali ya Nyamira zisitishwe
KUNDI moja la wakazi wa Nyamira wamewasilisha ombi kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wakipendekeza shughuli za serikali za kaunti hiyo zisitishwe kwa muda.
Ombi hilo lililopokelewa na tume hiyo Alhamisi liliwasilishwa na wakazi wanne kupitia kampuni ya mawakili ya Dennis Onyango Advocates.
Bw Jeremiah Migosi, Bw Astarico Omariba, Bi Ombati Eunice na Bw Jared Nyaribo wanataka serikali hiyo izimwe kwa muda kwa misingi ya masuala matatu waliotaja kama yenye uzito.
“Wateja wetu ni wakazi wa Kaunti ya Nyamira. Tungependa kukujulisha kuhusu nia yao ya kukusanya sahihi kuhimili ombi lao kwamba shughuli za serikali ya kaunti ya Nyamira zisitishwe kwa muda. Hii ni kutokana na hitaji la Kipengele cha 192 (1) cha Katiba likisomwa pamoja na kifungu cha 123 cha Sheria ya Serikali ya Kaunti Nambari 17 ya 2012,” ombi hilo linasema.
Wakazi hao wanadai kuwa serikali hiyo imehusika katika visa vya matumizi mabaya ya fedha na vitendo vinavyoenda kinyume na masilahi ya wapiga kura katika kaunti ya Nyamira.
Aidha, wanadai shughuli za utoaji huduma katika kaunti ya Nyamira zimelemazwa kutokana na kudhulumiwa kwa wafanyakazi.
“Wafanyakazi huwa hawalipwi kwa wakati hali inayowavunja moyo. Hawawezi kulalamika waziwazi kwani wanahofia kuchukuliwa hatua kali ikiwemo kupigwa kalamu,” walalamishi hao wakasema.
Vile vile, walidai kuwa Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo amekuwa akijilipa mshahara mkubwa na haramu ambao walisema ni kima cha Sh6.5 milioni kwa mwezi.
Lakini Bw Nyabiro amewahi kujitetea akisema kuwa kiasi hicho kinajumuisha baadhi ya malimbikizi ambayo hakuwa amelipwa hapo nyuma.
Sehemu ya malimbikizi hayo, akaeleza, ni pesa ambazo hakulipwa kwa muda wote aliohudumu kama Naibu Gavana.
Walalamishi hao pia wameorodhesha masuala kama utepetevu, usimamizi mbaya wa shughuli, kutolipwa kwa wafanyakazi vibarua kwa wakati, ukosefu wa vifaa vya kimsingi na dawa katika hospitali, kudorora kwa huduma za usambazaji maji, uchafu masokoni, uajiri wa wafanyakazi kwa mapendeleo na kukithiri kwa ufisadi.
Wametaja haya kutetea ombi lao la kutaka serikali ya kaunti ya Nyamira isimamishwe kwa muda.