• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
LAMU: Vijana kufadhiliwa baada ya kuhitimu masomo

LAMU: Vijana kufadhiliwa baada ya kuhitimu masomo

NA KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya kaunti ya Lamu itawanunulia vifaa vya kuanzisha kazi vijana wote wanaomaliza masomo ya vyuo vya ufundi kama njia mojawapo ya kuwavutia vijana zaidi kujiunga na vyuo hivyo kote Lamu.

Akihutubia umma wakati wa hafla ya ufunguzi wa ukumbi wa kisasa pamoja na kituo cha mawasiliano na teknolojia katika chuo cha kiufundi cha Lamu, Gavana wa eneo hilo, Fahim Twaha, aliwahimiza vijana kujiunga na vyuo vya kiufundi ili kujipatia ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa kwenye mradi unaoendelea wa ujenzi wa Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET).

Bw Twaha alisema serikali ya kitaifa inalenga kuendeleza miradi mikubwa eneo la Lamu na akasisitiza haja ya jamii ya eneo hilokuzingatia masomo ili kunufaika moja kwa moja na miradi hiyo.

Alisema serikali ya kaunti itajitahidi kuinua hadhi ya vyuo vya kiufundi kote Lamu, ikiwemo kuajiri walimu zaidi wa kufunza kwenye vyuo hivyo.

Aliipongeza serikali ya kitaifa kupitia kwa Rais Uhuru Kenyatta kwa kutoa Sh 15,000 kwa kila mwanafunzi anayejiunga na chuo cha kiufundi eneo hilo.

Gavana wa Lamu, Fahim Twaha akifungua kituo cha Mawasiliano na teknolojia cha Chuo cha Kiufundi cha Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

“Tayari tumepokea fedha hizo na kuzigawanya kwa wanafunzi husika. Pia tunalenga kuwafadhili vijana wote wanaomaliza masomo ya chuo cha ufundi kwa vifaa maalum vya kutekelezea kazi zao kulingana na ujuzi waliopata chuoni. Vifaa hivyo vitawawezesha kuanzia maisha na ningeomba mpatapo vifaa hivyo msikimbilie kuviuza,” akasema Bw Twaha.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa chuo cha ufundi cha Lamu, Ali Shebwana, alifichua kuwa chuo hicho kimeongeza zaidi idadi ya kozi zinazofunwa chuoni humo.

Bw Shebwana alisema kozi mpya zinazotolewa zinahusiana na taaluma ya masuala ya bandari ili kuwawezesha wanaohitimu chuoni humo kupata kazi kwa haraka katika LAPSSET.

“Awali tulikuwa tukitoa kozi za ujenzi, ulimbwende, ujuzi wa kuchomelea, ususi nakadhalika. Kwa sasa tumeongeza kozi, ikiwemo zile za masuala ya bandari, unahodha, uogeleaji wa kupiga mbizi miongoni mwa kozi nyingine. Yote haya tunayafanya ili kuwawezesha wanafunzi wanaohitimu kupata kazi katika LAPSSET,” akasema Bw Shebwana.

You can share this post!

Tutapendekeza wanawake watengewe 50% ya nafasi za uongozi...

Wakurugenzi kizimbani kwa ulaghai wa shamba la Sh54 bilioni

adminleo