Habari za Kitaifa

CBC kufunza uchumi wa majini kuchumia nchi Sh500 bilioni kwa mwaka


SERIKALI itajumuisha mafunzo kuhusu masuala ya majini katika mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC) ikilenga kuchuma jumla ya Sh500 bilioni kwa mwaka kutokana na uchumi wa majini kufikia mwaka wa 2035.

Vile vile, mtaala wa mafunzo ya walimu wa kufundisha elimu ya majini utafanyiwa mabadiliko ili kujumuisha masuala yatakayofanya wahitimu kupata ajira kwa haraka.

Hayo yalisemwa Alhamisi na Waziri wa Elimu Julius Migos alipofanya ziara ya kikazi katika kaunti ya Murang’a.

Alibashiri kuwa sekta ya uchumi wa majini ina uwezo wa kuzalisha angalau nafasi 200,000 za ajira kila mwaka.

Waziri alisema wakati huu, sekta hii inachangia asilimia 2.5 ya jumla ya utajiri wa Kenya na mapato ya kima cha Sh179 bilioni kila mwaka.

Bw Migos alisema Shule ya Pioneer Group of Schools iliyoko kaunti ya Murang’a inayomilikiwa na bwanyenye Peter Munga, imethibitisha kuwa kujumuishwa kwa mafunzo ya majini katika mtaala unasaidia katika kuvuna manufaa ya sekta hiyo.

“Shule hiyo imekuwa ikitoa mafunzo ya masuala ya majini na manufaa tayari yanaonekana. Idadi kubwa ya wanafunzi wamefaulu kujiunga na vyuo vikuu vya hadhi ya juu duniani kusomea shahada mbalimbali katika taaluma hii,” Bw Migos akasema.

Bw Munga, ambaye pia ndiye mwasisi wa Benki ya Family, alisema amegundua mchango wa elimu ya majini katika uchumi wa dunia na ndiyo maana ameshirikisha mtaala wake katika shule anazomiliki.

“Ni furaha yetu kwamba sasa serikali inalenga kushirikisha kozi za masuala ya majini katika mtaala wa CBC. Tunafurahi kuwa tunashirikishwa na kwamba shule yetu ya upili ndiyo ya kwanza kutoa mafunzo ya masuala ya majini nchini Kenya,” akasema.

Bw Munga alisema ameingia ubia na Bandari ya Mombasa na Kikosi cha Wanajeshi wa Majini kutoa nafasi ya mafunzo ya kiutendaji kwa wanafunzi wa shule zake.

Alisema wanafunzi wake hujifunza masuala ya ubaharia, viumbe wa majini, ufugaji samaki miongoni mwa masuala mengine katika bandari ya Mombasa