Ranchi yatafuta vyeti 400 vya ardhi vilivyoibwa kituoni mwa polisi Kajiado
ZAIDI ya vyeti 400 vya umiliki ardhi vilivyotwaliwa na vijana waliojihami vikali katika kituo cha polisi cha Kimana, Kaunti ya Kajiado wiki jana bado havijapatikana.
Vyeti hivyo vya umiliki ardhi, ni vya ranchi ya Imbirikani ambavyo wanachama wake wamekuwa wakizozonia uongozi.
Vyeti vyenyewe vilikuwa katika kijisanduku cha chuma ambacho vijana hao walichukua na kutoroka nacho baada ya kuvamia kituo hicho mnamo Agosti 24.
Mnamo Jumapili, Kamanda wa Polisi wa Kajiado Kusini David Maina alisema bado hawajapata kijisanduku hicho. Mwenyekiti wa ranchi hiyo Daniel Metui alikuwa amewapa polisi kijisanduku hicho baada ya kupata habari kuwa kundi la vijana lilikuwa limepanga kuvamia boma lake kukichukua.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, vijana hao waliokuwa wamejawa na hamaki walifika kwa fujo katika Kituo cha Polisi cha Kimana. Waliwalemea polisi na kuchukua kijisanduku hicho kisha wakaenda nacho kusikojulikana.
Bw Maina mnamo, Jumanne wiki jana, alisema kuwa walipata habari zilizodokeza kuwa kijisanduku hicho kilisafirishwa kwa gari usiku kwenye barabara ya Emali-Loitoktok.
Hata hivyo, hawakuweza kufikia gari hilo kwa sababu lilikuwa likisindikizwa na magari mengine matano kisha likayoyomea na kuwahepa karibu na bustani ya Milima ya Kyuhu.
“Tulijaribu kufuata gari hilo lakini likatuhepa. Vijana nao walikuwa wameanza kujikusanya kukabili maafisa wa polisi ambao hawakuwa na budi ila kukoma kuendelea na kulifuata gari lenyewe,” akasema Bw Maina.
“Tunashuku kuwa kijisanduku hicho kinahifadhiwa kwenye ranchi ya kibinafsi karibu na Kyulu,” akaongeza.
DCI imeanza uchunguzi
Afisa huyo alisema kuwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imeanzisha uchunguzi na washukiwa kadhaa wametambuliwa. Washukiwa hao watafikishwa mahakamani kwa makosa ya wizi wa kimabavu na kuvuruga kituo cha polisi.
Kwa mujibu wa Bw Metui, kutoweka kwa stakabadhi hizo ni pigo kwa wanachama wa ranchi hiyo ambao walikuwa na matumaini ya kupata vyeti vyao vya ardhi.
“Stakabadhi hizo zilichukuliwa kutoka kituo cha polisi, eneo ambalo limelindwa. Hii ni kama kuwanyima wanachama haki ya kumiliki vyeti vyao vya ardhi,” Bw Metui akaambia Taifa Leo.
Mnamo Jumamosi, utawala wa kaunti uliwakashifu Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja wakiwataka wawili hao waingilie kati suala hilo.
Kaunti ilitoa malalamishi kuwa Naibu Kamishina wa Kaunti (DCC) na Afisa wa ngazi ya juu katika kituo cha polisi cha Kimana walihusika na kupotea kwa vyeti hivyo vya ardhi.
Gavana Joseph Ole Lenku, Seneta Samuel Seki, Seneta Mteule Peris Tobiko, wabunge Samuel Parashina (Kajiado Kusini), Onesmus Ngogoyo (Kajiado Kaskazini) walimtaka Waziri wa Usalama Profesa Kithure Kindiki na Bw Kanja kumwaadhibu kamishina wa kaunti na polisi wa kituo cha Kimana.
“Tumechoka na kuna afisa wa ngazi ya juu serikalini kutoka eneo hili ambaye anatumia mamlaka yake vibaya na kuwatishia polisi. Hatutamvumilia zaidi,” akasema Bw Lenku.
Bw Ngogoyo alisema inashangaza kuwa kijisanduku hicho kilipotea katika kituo cha polisi na hakuna mtu yeyote ambaye amenyakwa.
“Polisi wanavurugwa na wanasiasa wanaoegemea mrengo wa UDA,” akasema.
Juhudi za kumngóa Bw Metui na baadhi ya wanachama wa ranchi hiyo zimekosa kuzaa matunda kwa sababu korti imetoa uamuzi unaopinga juhudi hizo.
Bw Metui anaegemea mrengo wa Lenku huku Konee Kinyaku anayeegemea mrengo wa Mkuu wa Wafanyakazi Ikulu Katoo Ole Metito pia akipigania uongozi wa ranchi hiyo.