Habari za Kitaifa

Maoni: Ziara ya Ruto Nyanza ilijaa siasa tupu, hakuna la mno! 

Na CECIL ODONGO September 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ZIARA ya Rais William Ruto Nyanza ilikuwa na ajenda ya kisiasa iliyolenga kutathmini kama eneo hilo lipo nyuma yake baada ya ODM kumnusuru kutoka kwa ghadhabu za Gen Z.

Kinyume na dhana ambayo inaendelezwa kuwa ziara hiyo ilikuwa ya maendeleo, hakuna mradi wowote mpya ambao ulizinduliwa na Rais Ruto.

Kuonyesha kuwa ziara hiyo ilikuwa tu ya kisiasa, katika kila mkutano aliohotubu Rais, jina la Raila lilikuwa likitajwa huku akisifiwa kutokana na uamuzi wake wa kushirikiana na serikali.

Raila anaendea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) na tayari Rais Ruto ameweka wazi kuwa serikali yake itaendeleza kampeni kabambe kuhakikisha anatwaa nafasi hiyo.

Wandani wa Raila nao waliahidi kuwa watamuunga mkono Rais mradi tu ashirikiane na Raila kuelekea uchaguzi wa 2027.

Kilichokuwa dhahiri katika ziara hiyo ni kuwa huenda Rais ametanabahi kuwa eneo la Mlima Kenya halitamuunga mkono tena ndiposa sasa ameamua kuchangamkia ngome za ODM.

Aidha, ili kuonyesha kuwa ziara hiyo haikuwa ya maendeleo, miradi iliyozinduliwa ilisalia tu na majukwaa ya kupiga siasa za 2027 na kumshukuru Rais kwa kumkumbatia Bw Odinga.

Mradi wa Sola katika kisiwa cha Mageta eneobunge la Bonde ulianzwa mnamo 2019 wakati wa utawala wa handisheki na ulikuwa umekamilika.

Pia, katika Kaunti ya Siaya alifungua kiwanda cha kusaga mpunga cha Siriwo, mradi ambao ungeweza kufunguliwa na hata serikali ya gatuzi hilo.

Katika Kaunti ya Homa Bay, ujenzi wa soko la kisasa la samaki mjini Homa Bay umekuwa ukiendelea na unaelekea kukamilika.

Katika Kaunti ya Migori, Rais alitoa tu ahadi kuhusu mradi wa unyunyuziaji mashamba maji eneo la Kuja.

Mradi huo haujaanzishwa, na ufanisi wake utatagemea tu iwapo utakamilishwa.

Kituo cha Kupambana na Matatizo ya Kisaikolojia cha Nyabondo katika eneobunge la Nyakach, si mradi mpya na hata taasisi yenyewe ya kimatibabu imekuwepo kwa miaka mingi.

Ni dhahiri kuwa hakuna mradi wowote mpya ulizinduliwa katika ziara hiyo Dkt Ruto Nyanza.

Ilikuwa tu hafla ya ya kuhudhuria makaribisho ya nyumbani ya mawaziri John Mbadi (Fedha) na Opiyo Wandayi (Kawi).

Viongozi wa Nyanza nao waliwafeli wananchi kwa kutozungumzia masuala ya kimsingi na badala yake wakachapa tu siasa za Raila na Ruto.

Wanasiasa hao hawakuzungumzia matatizo yanayoathiri sekta ya miwa, ilhali viwanda vingi vya sukari vinaendelea kuporomoka.

Hakuna chochote kilichozungumziwa kuhusu bwawa la Soin-Koru huku mafuriko nayo yakiendelea kutesa wakazi wa Nyando kila kukicha.

Wakati wa maandamano, wale ambao wameumia mno ni wakazi wa Nyanza kutokana na uaminifu wao kwa Raila.

Inashangaza kuwa wahanga wa ghasia baada ya uchaguzi kutoka Nyanza hawajawahi kufidiwa huku wenzao kutoka maeneo ya Kati na Bonde la Ufa wakilipwa.

Katika eneobunge la Nyakach, kumekuwa na mzozo wa mipaka na wizi wa mifugo eneo la Sondu, na hakuna chochote kilichozungumziwa kuhusu hili.

Kwa hivyo, hakuna chochote cha kujivunia kuhusu ziara ya Ruto Nyanza na iwapo kuna yale yaliyoafikiwa kwenye mkutano na viongozi katika Ikulu ya Kisumu, basi yawekwe wazi ili wananchi wayafahamu.