AG Oduor kutetea Ruto kortini Arusha kesi ya kudhulumu Gen Z wakati wa maandamano
BUNGE la Mwananchi limewasilisha kesi dhidi ya viongozi wakuu serikalini, akiwemo Rais William Ruto, katika korti ya Afrika Mashariki kutetea haki za kibinadamu iliyoko nchini Arusha, Tanzania, kufuatia malalamishi ya vijana wa Gen Z.
Kesi hiyo inahusu ukiukaji wa haki za kibinadamu wakati wa maandamano ya vijana maeneo mbalimbali nchini.
Wengine wanaotajwa kwenye kesi hiyo ni pamoja na naibu rais Rigathi Gachagua, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu (AG) Justin Muturi, Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki, na aliyekuwa Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi, IG Japhet Koome.
Bunge la Mwananchi ni mojawapo ya mavuguvugu yanayotetea haki za kibinadamu nchini, na kukosoa serikali tawala inapoenda mrama.
Akizungumza baada ya kurejea nchini Septemba 2, 2024, Rais wa vuguvugu hilo, Francis Awino alisema kuwa wamechukua hatua kama njia mojawapo ya kutafuta haki kwa waathiriwa wa maandamano.
“Tumeamua kuwasilisha kesi hiyo ili waathiriwa wote wa maandamano ya Gen Z hasa wale waliouawa, kutekwa nyara na kujeruhiwa wapate haki,” Awino alisema.
Korti hiyo imeipa serikali ya Kenya siku 45 kuipa majibu.
Akijibu hatua iliyochukuliwa na Bunge la Mwananchi, Mwanasheria Mkuu mpya, Dorcas Oduor alisema kuwa atawakilisha wote walioshtakiwa katika korti ya Afrika Mashariki kuhusiana na maandamano hayo.
“Nitashughulikia yale yote yaliyowasilishwa kwenye ofisi yangu mojawapo ikiwa ni kesi iliyowasilishwa kwenye korti ya Afrika Mashariki,” akasema Bi Oduor.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya vuguvugu hilo kutoa wito kwa serikali ya Kenya Kwanza iwafidie waathiriwa wa maandamano.
Bw Awino kwenye kesi hiyo anaishutumu serikali kwa kutumia nguvu kupita kiasi, maafisa wa polisi kuwaua waandamanaji na ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu
“Serikali inafaa kufidia waathiriwa wote wa ukatili wa polisi. Kuna wale ambao walijeruhiwa, wengine waliuawa. Familia ya waliouawa inafaa kufidiwa pia,” akasema Bw Awino.
Kando na hayo, aliitaka serikali kuzingatia Katiba ya Kenya na kukoma kudhulumu raia.
“Wakati wa maandamano, vijana wa Gen Z walikuwa wakiandamana bila vurugu. Hata hivyo, polisi walitumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya jambo ambalo lilifanya mamia kuumia na wengine kupoteza maisha yao,” akaongeza.