Habari za Kitaifa

AUC: Ruto avumisha Raila kwa marais sita wa Afrika, kule Beijing  

Na CHARLES WASONGA September 4th, 2024 1 min read

RAIS William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga Jumatano, Septemba 4, 2024 walifanya mazungumzo na marais kadhaa wa Afrika pembezoni mwa Mkutano kuhusu Ushirikiano wa China na Afrika (FOCAC) jijini Beijing, China.

Kulingana na taarifa kutoka kitengo cha habari za rais (PPS) Rais Ruto alijadili masuala yanayohusiana na ushirikiano kati ya Kenya na nchi za Afrika.

“Rais Ruto pia alitumia nafasi hiyo kumpigia debe Bw Odinga ambaye ni mgombeaji wa Kenya katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC),” ikasema taarifa hiyo.

Jumatano, Rais Ruto na Odinga walifanya mikutano tofauti na marais kama vile Faure Essozimna Gnassingbé wa Togo na Assimi Goita (Mali), Paul Kagame (Rwanda), Umaro Sissoco Embalo (Guinea-Bissau), Mahamat Idriss Deby (Chad) na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema.

Rais Ruto alielezea kujitolea kwa Kenya kuimarisha uhusiano na nchi hizi kwa manufaa ya raia wa taifa hili.

Alisema Kenya itatafuta njia za kuimarisha uhusiano na nchi hizo katika nyanja za kidiplomasia, biashara na mahusiano ya raia wa nchi hizo na Wakenya.

“Hii ndio maana viongozi wa Afrika wanashirikiana kufanya mageuzi katika Umoja wa Afrika (AU) ili iweze kuhudumia bara hili katika nyanja mbalimbali za kiuchumi,” Dkt Ruto akasema.

“Kwa hivyo, Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ni asasi muhimu ya AU inayohitaji kuongozwa na mtu mwenye ufahamu kuhusu changamoto zinazozonga Afrika na namna ya kukabiliana nazo,” akaongeza.