Habari za Kitaifa

Wajakazi kizimbani kwa wizi wa Sh30.7 milioni

Na RICHARD MUNGUTI September 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAFANYAKAZI wawili wa nyumbani ‘watajua hawajui’ endapo hawatafichulia polisi katika kipindi cha siku tano jinsi walivyomwibia mwajiri wao Sh30.7milioni katika kipindi cha miaka miwili.

Akiruhusu polisi wawazuilie Felistas Nyambura na James Wachira waliomfanyia kazi Joseph Barage Wanjui, hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi mnamo Ijumaa Septemba 6,2024 alisema, “Uchunguzi wa kina wahitaji kufanywa kubaini jinsi washukiwa hao walitekeleza uhalifu huo.”

Hakimu alielezwa na kiongozi wa wa mashtaka Bi Virginia Kariuki kwamba Joseph Barage Wanjui alifariki miezi michache iliyopita.

Bw Ekhubi alifahamishwa na Bi Kariuki kwamba washukiwa hao walikuwa wameajiriwa kama mjakazi na dereva na Bwana na Bibi Wanjui.

Kiongozi huyu wa mashtaka alieleza hakimu kwamba wizi kutoka akaunti ya Bw Wanjui iliyoko Absa Bank Kenya PLC uligunduliwa na maafisa wa uhalifu wa kimitandao katika Benki Kuu ya Kenya.

Polisi waligudua Sh706,000 ziliibwa kutoka kwa akaunti ya Wanjui.

Wawili hao walisakwa na kupatikana katika makazi ya Wanjui jijini Nairobi.

Walitiwa nguvuni  Septemba 3 baada ya mjane wa Wanjui kuelezwa na maafisa wa polisi wa BFIU kufichua wizi kutoka kwa akaunti ya Bw wanjui.

Walizuiliwa katika kituo cha polisi cha Spring Valley, Nairobi kisha Koplo Michael Wandera kufika kortini kuomba muda wa kuwazuilia kwa siku 14 na kuwahoji.

Mahakama iliombwa iwazuilie wafanyakazi hao wa Bw Wanjui kwa siku 14 kuwezesha polisi kusafiri hadi kaunti za Mombasa, Meru, Nakuru mbali na Nairobi kupokea ushahidi.

Wanataka ushahidi kutoka kwa vituo vya kuuza petrol ambako kadi ya benki ya Wanjui ya Credit Card ilitumika kutoa pesa katika akaunti yake iliyoko Absa Bank.

Akiwasilisha ombi hilo la kuzuiliwa kwa washukiwa kwa siku 14, Koplo Michael Wandera alisema anahitaji muda wa kurekodi taarifa kutoka kwa maafisa wa benki, watu wa familia ya marehemu Wanjui na kupata video kutoka kwa kamera za CCTV.

Polisi pia waliambia mahakama watawasimamisha katika foleni washukiwa hao watambuliwe na mashahidi.

Mawakili wawili wanaowatetea washukiwa hao walipinga muda wa siku 14 wa polisi kuwahoji wawili hao.

Hakimu alipunguza muda wa siku 14 kwa siku tisa (9). Sasa watahojiwa kwa siku  tano. Watarudishwa kortini Septemba 11,2024.