Habari za Kitaifa

‘Mimi ni chuma ya zamani, Raila hanitishi serikalini,’ asema Gachagua

Na ROSELYNE OBALA September 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amekana madai kwamba ushawishi wake unatishiwa na ujio wa wandani wa Raila Odinga ndani ya serikali ya Kenya Kwanza, akisema nafasi yake ni thabiti na inalindwa.

Bw Gachagua pia amepuuzilia mbali madai kuwa ushawishi wake Mlima Kenya unatishiwa na wabunge wa eneo hilo wanaompinga, wakipigwa jeki na wenzao wanaoegemea mrengo wa Bw Odinga.

Naibu Rais alikuwa akimjibu kiongozi wa chama cha Democratic Action Party (DAP) Eugene Wamalwa aliyeuliza ikiwa ametikiswa na hatua ya Rais William Ruto kuteua viongozi wa ODM kuwa mawaziri.

“Usiwe na wasiwasi kuhusu nafasi yangu katika serikali. Mimi ndiye mwenyewe na niko ndani. Hata waje akina nani, mimi ni chuma ya zamani sitishiki,” Bw Gachagua alisisitiza.

Alikuwa akiongea mjini Kitale, kaunti ya Trans Nzoia katika hafla ya mazishi ya aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Kupambana na Pombe na Mihadarati (Nacada) Victor Okioma.

“Niko ndani. Hii ni serikali niliyopigania. Siwezi kuenda popote, siwezi kusonga hata nchi moja. Tumewakaribisha wale Rais aliwaleta serikalini,” akaeleza Bw Gachagua.

Viongozi wa ODM walioteuliwa kuwa mawaziri serikalini ni  Hassan Ali Joho ambaye ni Waziri wa Uchumi wa Majini, John Mbadi (Waziri wa Fedha), James Opiyo Wandayi (Kawi), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika) na Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Beatrice Askul Moe.

Baadhi ya wabunge wa kutoka Mlima Kenya wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah wamekuwa wakimshambulia Bw Gachagua, wakiapa kumtetea Bw Odinga na mawaziri hao watano.

Bw Ichung’wah ambaye ni Mbunge wa Kikuyu ameapa kutomwogopa Naibu Rais akijitapa alimkabili Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alipokuwa mbunge bila cheo chochote serikalini.

“Hauwezi kunitisha kwa sababu uko karibu na rais. Nilimpiga vita Rais Kenyatta. Naogopa Mungu, uji moto na stima pekee. Na mtu asituambie kwamba tusingemkaribisha Raila huku akituuzia woga na ukabila,” Bw Ichung’wah alisema akiwa Rongai.

Na akiwa Kitale, Bw Gachagua alisema hawezi kutikiswa na yeyote.

“Hata kama walijaribu kuandaa hoja ya kuniondoa afisini, hawakuweza kwa sababu yule anayeshikilia wadhifa wa Naibu Rais ni Riggy G-Chuma. Hali ni hivyo, hatuna shida sisi tunataka Wakenya wote waungane,” Naibu Rais akasema alisisitiza kuwa ataendelea kushinikiza umoja wa Mlima Kenya “kwa sababu watu wengine wanafanya hivyo katika maeneo yao.”

Bw Wamalwa alitoa kumbukumbu kuhusu jinsi ushindani wa kisiasa ulishuhudiwa katika eneo la Magharibi mwa Kenya; kati ya miungano ya Azimio na Kenya Kwanza.

Alisema kuwa Gavana wa Bungoma Ken Lusaka na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula waliibuka washindi katika kaunti ya Bungoma na chama chake cha DAP-K kikashinda kiti cha ugavana wa Trans Nzoia kupitia Gavana George Natembeya.

Bw Wamalwa, hata hivyo, alimwambia Naibu Rais kwamba dalili zinaonyesha kuwa “mchezo ni ule ule lakini wachezaji wamebadilisha timu zao.”

“Tuko na marafiki katika Azimio ambao wamebadilika na kujiunga na serikali. Siasa hazitabiriki, zinabadilika kila mara,” akasema, akimhimiza Bw Gachagua kuwa mwangalifu asiendeshe siasa bila kuwa na mikakati.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga