Habari za Kaunti

Haja ya kuinua mitaa ya mabanda kielimu

Na CECIL ODONGO September 8th, 2024 1 min read

ALIYEKUWA Waziri Msaidizi wa Elimu Dkt Sarah Ruto amesema juhudi zinahitaji kuelekezwa kuimarisha elimu hasa kwa wanafunzi wanaoishi katika mitaa ya mabanda maeneo mbalimbali nchini.

Dkt Ruto amesema kuwa  kuna changamoto nyingi ambazo zinawaathiri wanafunzi katika mitaa hiyo na nguvu zisipoelekezwa katika kuhakikisha wanapata elimu, wengi wao wataishia  kupotoka kimaadili.

“Kunahitajika sera ambapo wanafunzi wanaoishi kwenye mitaa ya mabanda watapata elimu badala ya kuachwa kupotoka. Maisha kwenye mitaa ya mabanda ni magumu mno na wengi wa watoto huishia kupotea na kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya au wizi,” akasema Dkt Ruto.

Alikuwa akizungumza katika mtaa wa mabanda wa Mathare wakati ambapo aliongoza shughuli za kutoa sare na viatu kwa wanafunzi 602 kutoka shule saba mtaani humo.

Msaada huo ulitolewa na Shirika lisilo la kiserikali la SHOFCO ambalo linafahamika kushiriki miradi ya kuinua jamii kwenye mitaa ya mabanda maeneo mbalimbali nchini.

Shule ambazo zilipokea msaada huo ni zile ambazo ziliathiriwa na mafuriko makubwa ambayo yalitokea mnamo Aprili na Mei mwaka huu na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundomsingi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Elimu Ukanda wa Nairobi Dkt Margaret Lesuuda na Mkurugenzi wa Mipango na Mikakati wa Shofco Mark Laichena.

Dkt Lesuuda alisema kuwapa wanafunzi hao sare na viatu ilikuwa hisani ambayo itawapa motisha ya kumakinikia masomo yao.

“Wamepata matumaini kuwa kuna watu ambao wanawajali hasa ikizingatiwa waliathiriwa na mafuriko na pia maisha katika mitaa ya mabanda huandamana na changamoto tele,”akasema Dkt Lesuuda.

Bw Laichena naye alisema Shofco itazidi kupambana na umaskini kwenye mitaa ya mabanda akisema miradi mingi wanayoitekeleza inalenga kuinua maisha ya wanaoishi kwenye mitaa hiyo.