Habari

Hali tete Gavana Wavinya akikanusha alizuiliwa Uingereza kwa ulanguzi wa pesa

Na KITAVI MUTUA September 10th, 2024 1 min read

GAVANA wa Machakos Wavinya Ndeti  amekanusha madai kwamba amekuwa akizuiliwa kule Uingereza kwa madai ya ulanguzi wa fedha.

Bi Ndeti amekuwa nje ya nchi tangu Agosti 30 na kumekuwa na madai mitandaoni  yanayohusiana na usalama wake na ya familia yake.

Ingawa hivyo, gavana amesema kuwa hajakamatwa au mwanafamilia yake yeyote kuzuiliwa London kwa tuhuma za ulanguzi wa fedha.

Alisema wale ambao wamekuwa wakidai alikamatwa akiwa na mabunda ya mamilioni ya pesa ni wale ambao wanaenza chuki na ni maadui wake wake wa  kisiasa.

“Wale ambao wanaeneza habari feki hawafahamu chochote kuhusu sheria za Uingereza na asasi za fedha za huko. Nawahakikishia kuwa mimi na familia yangu tuko salama na hatuna shida zozote nyumbani na ugenini,” akasema Bi Ndeti kupitia taarifa.

Pia gavana huyo aliwaonya wale ambao wamekuwa wakieneza ‘habari hizo feki’ dhidi yake na familia yake, watakabiliwa kisheria.

“Tunawajua wale ambao wanaeneza habari hizo na hii ni kuharibia mtu sifa. Madai yao yameleta dhana mbaya kunihusu na familia yangu,” akaongeza Bi Ndeti.

Naibu Gavana Francis Mwangangi naye alisema bosi wake alikuwa  ameenda Uingereza kwa ziara rasmi na pia kumpeleka mwanawe asajiliwe katika chuo kikuu nchini humo.

“Niliandaa mazungumzo  na bosi wangu asubuhi na ninaweza kuwathibitishia watu wa Machakos kuwa gavana yuko salama na anatarajiwa kurejea Kenya mnamo Septemba 15,” akasema Bw Mwangangi.

Mnamo Ijumaa taarifa ilienea mitandaoni kuwa gavana na mwanawe Charlesa Oduwale walikuwa wamekamatwa London.

Wakenya wengi walishangaa jinsi pesa nyingi ambazo Bi Ndeti alidaiwa kuwa nazo zilipita kwenye nyuga mbalimbali za ndege.