Majonzi aliyekuwa waziri msaidizi akifariki
ALIYEKUWA Waziri Msaidizi wa Uchukuzi na Mbunge wa Bomachoge Chache Simon Ogari amefariki.
Familia ya Dkt Ogari ilisema alifariki Jumanne asubuhi nyumbani kwake Karen jijini Nairobi.
“Hayupo tena, alifariki mwendo wa saa kumi na moja asubuhi. Alikuwa akiugua kwa muda mrefu,” alisema mtu mmoja wa familia.
Mwingine aliongeza, “Polisi wapo hapa. Tutatoa maelezo zaidi mara tutakapomalizana nao.”
Jamaa walisema kuwa mbunge huyo wa zamani alikuwa akitafuta matibabu mara kwa mara hospitalini kwa miaka miwili iliyopita.
Dkt Ogari, 68, alikuwa mbunge wa eneobunge la Bomachoge katika Bunge la 10 na aliwakilisha Bomachoge Chache katika Bunge la 11.
Seneta wa Kisii Richard Onyonka aliomboleza marehemu Ogari akisema,” alikuwa mtu mwenye adabu, mkarimu na asiye na ubinafsi.”
“Mbali na kuwa kiongozi mzuri na mfanyakazi mwenzangu, alikuwa rafiki yangu wa kibinafsi kwa miaka mingi. Alikuwa mtu mzuri ambaye mimi binafsi nitamkosa katika kifo chake.”
Seneta huyo alisema kuwa kujitolea kwa Dkt Ogari kuhudumia watu wa Bomachoge kutasalia kuwa mfano bora kwa “sisi sote katika uongozi”.
“Ogari alifanya kazi bila kuchoka kuinua maisha ya wapiga kura wake, na mchango wake kwa jamii yetu hautasahaulika. Tunapoomboleza msiba huu mkubwa, natuma rambirambi zangu kwa familia yake, marafiki na watu wa Bomachoge,” alisema Bw. Onyonka.