Sababu za Maaskofu 50 kutetea Gachagua
ZAIDI ya maaskofu 50 kutoka Nyandarua wametoa wito wa kukomeshwa kwa mizozo ya kisiasa kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na viongozi wengine wa Kenya Kwanza.
Katika hotuba ya pamoja kwa wanahabari katika Kituo cha Hope Impartation Centre katika Mji wa Nyahururu mnamo Jumanne, maaskofu, wakiongozwa na Askofu Mkuu Josam Kariuki, waliamua kuunga mkono mpango wa Naibu Rais wa kuunganisha eneo la Mlima Kenya.
Maaskofu hao chini ya Baraza la Dini Mbalimbali la Nyandarua walielezea wasiwasi wao kuhusu mizozo ya wazi ya kisiasa, na kuwataka viongozi kuheshimu na kuunga mkono juhudi za Bw Gachagua kuunganisha eneo hilo.
‘Inasikitisha viongozi wa kisiasa wanapoingia kwenye mitandao ya kijamii au majukwaa ya kisiasa kupigana wenyewe kwa wenyewe. Wanasiasa lazima waache ubinafsi, waheshimiane, na kutatua tofauti zao mbali na macho ya umma. Tunaunga mkono wito wa Naibu Rais Gachagua kuunganisha eneo la Mlima Kenya kwani ndiyo njia pekee tunaweza kufaidika na ajenda ya maendeleo ya serikali kama jamii, alisema Askofu Mkuu Kariuki.
Askofu huyo mkuu alisisitiza zaidi kwamba viongozi wa eneo hilo wanapaswa kuiga mfano wa Rais William Ruto wa kuwakumbatia wanasiasa wa ODM, hatua ambayo imesaidia kuunganisha nchi.
“Ikiwa Rais Ruto amemkumbatia Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga, kwa nini viongozi wa Mlima Kenya hawawezi kufanya vivyo hivyo kwa kuunga mkono na kufanya kazi na nao.”
Pia alionya kuwa migogoro ya kisiasa hutuma ujumbe usio sahihi kwa umma, akitoa wito kwa viongozi kushughulikia mizozo katika vikao vya faragha.
“Inaonyesha taswira mbaya kwa jamii wakati viongozi wanapokosoana hadharani. Ikiwa kiongozi hatekelezi wajibu wake, acha wengine wahutubie katika majukwaa mengine nje ya jukwaa la umma,” alisema Askofu Mkuu Kariuki.
Maaskofu hao pia wameeleza umuhimu wa viongozi kusikiliza jamii ili kuepuka kuzidisha mivutano ya kisiasa.
Walielezea wasiwasi wao juu ya maandamano ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na yale yaliyopangwa na wanafunzi wa chuo kikuu kuhusu mfumo mpya wa ufadhili.
‘Tumekuwa na maandamano mengi mwaka huu kwa sababu wanasiasa hawashirikiani na jamii na wanatumia muda mwingi kupigana na naibu rais badala ya kusikiliza jamii,’ alisema Askofu Mkuu Kariuki.