Habari za Kitaifa

Bunge la Kaunti ya Nairobi kujadili mswada wa kudhibiti vyumba vya Airbnb

Na WINNIE ONYANDO September 11th, 2024 1 min read

DIWANI mteule katika Kaunti ya Nairobi, Perpetua Mponjiwa, amewasilisha mswada bungeni akipendekeza sheria kali ziwekwe za kudhibiti vyumba vinavyotumia mtandao wa Airbnb, haswa kutokana na visa vya mauaji ya wanawake vinavyoripotiwa katika vyumba hivyo.

Kulingana na diwani huyo aliyewasilisha mswada mnamo Jumanne Septemba 10, 2024, hatua hiyo itasaidia pakubwa katika kudhibiti visa vya mauaji kwenye vyumba hivyo.

“Ninapendekeza serikali kushirikiana na Wizara ya Utalii na Wanyamapori kuweka sheria kali za kudhibiti vyumba vya Airbnb kama njia ya kuwalinda akina dada,” akasema Bi Mponjiwa.

Kando na hayo, alipendekeza kuwa kamera za CCTV pia ziwekwe ili wanaoingia kwenye vyumba hivyo watambuliwe.

“Ikiwa ni mtu aliye na nia mbaya, basi atanaswa kwenye kamera ya CCTV,’ akaongeza.

Alisema kuwa kando na kutumika na Wakenya, vyumba hivyo pia vinatumika na watalii hivyo kuna haja ya kuvifanya viwe salama.

Mswada huo unajiri miezi michache baada ya serikali kutangaza kuwa itaandama wamiliki wa vyumba vya malazi visivyosajiliwa na hata vile vinavyotumia mtandao wa Airbnb kuendesha biashara hiyo.

Diwani mteule wa Kaunti ya Nairobi, Perpetua Mponjiwa. PICHA | WINNIE ONYANDO

Hatua hiyo ilifuata ongezeko la visa vya mauaji ya kinyama yanayotekelezwa katika vyumba hivyo kote nchini.

Kwenye taarifa ya pamoja waliyoituma kwa vyombo vya habari mnamo Februari, Katibu katika Wizara ya Usalama Raymond Omollo, Katibu wa Wizara ya Jinsia Anne Wang’ombe, Beatrice Inyangala (Elimu ya Juu) na John Olultuaa (Utalii) walisema operesheni dhidi ya vyumba hivyo visivyosajiliwa itaanza Februari 5, 2024.

Wanne hao waliwataka wamiliki wa vyumba hivyo kuhakikisha wamevisajili kwa Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Utalii Nchini (TRA) kabla ya maafisa wa serikali kuwafikia.