Imani kali ya kidini inavyochangia watu kujiua
IMANI potofu ya kidini imetajwa kuwa miongoni mwa sababu za kukithiri kwa visa vya matatizo ya kiakili na mafadhaiko yanayowasukuma watu kujiua hasaa wanapokumbwa na shida.
Mwanasaikolojia wa Murang’a Garrison Irungu anasisitiza kuwa waathiriwa hufichua kuwa wao huwa wanazungumza na Mungu kabla yao kujitenga na jamii na kuanza kusumbuka.
Viongozi wa kidini wanaposhindwa kuwasaidia, wao hufa moyo na kufadhaika.
Irungu ambaye anafanya kazi katika hospitali ya Murang’a Level-5 alibainisha kuwa badala ya watu walioathiriwa kutafuta usaidizi wa kitaalamu kuganga matatizo ya kiakili, wanageukia viongozi wa kiroho, ambao ushauri wao unaweza kuzorotesha hali yao ya kiakili bila kukusudia.
“Waathiriwa wengi wanaripoti kusikia jumbe kutoka kwa Mungu au ‘watu wengine wa Mungu’ na mara nyingi hutafuta uthibitisho kutoka kwa viongozi wao wa kiroho,” Irungu akasema.
Aliongeza, “Hata hivyo, viongozi hao wa kidini wanaposhindwa kushughulikia masuala ya kisaikolojia ya dhiki zao, watu hao huachwa na upweke. Kutengwa huko kunadhuru afya yao ya akili, na wakati mwingine kuwasababishia mawazo ya kujiua.
Kulingana na Irungu, kupuuza kipengele cha kisaikolojia kinachojikita katika dini kunaweza kuwa na matokeo mabaya.
“Waathiriwa mara nyingi hujitenga na marafiki na wanafamilia, wakiamini kuwa wamechaguliwa kwa mwito wa hali ya juu. Hali hii huwapotosha kabisa. Wakiachwa bila kutibiwa, upotofu huu unaweza kuongezeka, na kuwasukuma watu kukakaribia kujidhuru au kujiua,” alieleza Irungu.
Alibainisha kuwa ukosefu wa elimu ya namna ya kukabiliana na changamoto za afya ya akili pia huchangia ongezeko la wagonjwa wa afya ya akili.
Irungu alisema kuwa kuwekeza katika programu za uhamasishaji kunaweza kusaidia kupunguza unyanyapaa wa watu wanaokabiliwa na changamoto za afya ya akili.
Mpango huu utasaidia katika kuongeza kiwango cha wagonjwa kama hao wanaotafuta matibabu.
“Serikali ya kaunti ya Murang’a kupitia idara ya daktari wa akili katika hospitali ya Murang’a Level 5 imebuni mpango wa kuwafikia watu ambao hutoa ushauri nasaha na huduma za kiakili kwa waathiriwa waliokumbwa na maporomoko ya ardhi huko Gitugi wakati wa msimu wa mvua uliopita,” alisisitiza.
“Hii ilisaidia wakazi wengi waliopoteza wapendwa wao na mali katika tukio hilo. Hafla kama hizi zinafaa kupangwa mara kwa mara ili kuwafikia watu ambao wana matatizo ya kiakili,” alisema mwanasaikolojia huyo.
Aliendelea, “Kuna programu chache za uhamasishaji nchini za kushughulikia matatizo ya afya ya akili. Kuwa na programu nyingi kama hizi kutapunguza unyanyapaa unaohusishwa na masuala ya afya ya akili na kurahisisha watu kutafuta usaidizi wa kitaalamu.”
Irungu aliwahimiza watu kusaidia na kuwapeleka hospitalini wanajamii ambao wanaonyesha dalili za tabia isiyo ya kawaida ili kusaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wa afya ya akili.