• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
MURANG’A: Eneo ambako genge huitisha wenye magari Sh175,000 kuwaruhusu barabarani

MURANG’A: Eneo ambako genge huitisha wenye magari Sh175,000 kuwaruhusu barabarani

Na MWANGI MUIRURI

KWA miaka tisa sasa, wenyeji wa kaunti ndogo ya Kigumo katika kaunti ya Murang’a wameishi na ukweli kwamba genge linaweza likatwaa mamlaka ya serikali na liwe ni jambo la kawaida.

Hali hiyo wameishuhudia katika barabara ya kutoka kaharate kuelekea Kangari, barabara iliyo na urefu wa kilomita 41 ambayo iko katika udhibiti wa genge la vijana.

Vijana hao hutekeleza majukumu ya mamlaka ya uthibiti biashara ya uchukuzi wa umma (TLB) na pia yale ya mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA).

Na sio eti serikali kuu na ile ya Kaunti hazina ufahamu; La hasha, zina ufahamu huo lakini zimeligeuza kuwa suala la kawaida kiasi kwamba hata huonekana pamoja katika ushirika huu ni sawa na ule uhusiano wa chanda na Pete.

Uthibiti wa genge hilo hutekelezwa kwa msingi kuwa, magari yote ambayo hukubaliwa kufanya biashara katika barabara hiyo ni yale tu ambayo yamepewa idhini na genge hilo.

Sh175,000!

“Idhini hiyo huwa mmiliki wa gari hilo atoe Sh175, 000 kwa genge hilo, dereva ajisajili kwa Sh5, 000 na makanga Sh2, 500. Hatimaye, kila gari katika huduma barabarani hiyo linatoa Sh200 kila siku kwa genge hilo ili lipewe ulinzi dhidi ya magari mengine kuingia kufanya biashara,” asema mmoja wa wadokezi wetu katika sakata hii.

Kamishna wa kaunti ya Murang’a Mohammed Barre anakiri kuwa amepokezwa jumbe tele kuhusu genge hilo na mpangilio huo wa kusaka ukiritimba wa utumizi wa barabara na pia kuvuna pesa, lakini anakiri pia kuwa hana jibu la ni lini ujambazi huo utazimwa.

Ukiritimba wa aina hii ni miongoni mwa maovu ya kibiashara ambayo rais Uhuru Kenyatta alikemea akihutubia Taifa katika uwanja Wa Narok alipoongoza Taifa kuadhimisha makala ya 56 ya Madaraka Dei.

“Hali hii iko kama unavyoisema…Ndio kuna shida kubwa katika barabara hiyo..Lakini ni vigumu kuthibiti hali kwa kuwa hakuna walalamishi ambao hukubali kujitokeza kutupa habari kamili,” asema Barre.

Ingawa kuwa serikali kuu anayoisimamia katika Kaunti ya Murang’a imeajiri maafisa wa uchunguzi wa jinai (DCI) na pia wenzao wa ujasusi (NIS) kutekeleza usakaji wa habari za kusaidia serikali kuimarisha usalama, Bw Barre anasema kuwa “hili ni suala ngumu.”

Suala likiendelea kuwa ngumu kwa Kamishna Barre, genge hilo limeweka maeneo kadhaa ya kushirikisha sakata yao ambapo katika maeneo ya kaharate, Heho, Jikaze, kwa Mukangema, Gwa Kirore, Kwa Geoffrey, Muthithi nje ya kituo cha polisi cha Muthithi na pia katika eneo la Gakira huwa na vijana wa kuokota hizo Sh200 kutoka kwa kila gari.

Wafanyakazi wa serikali kuu waweka matuta katika eneo hili la barabara ya kutoka kaharati kwenda Kangari na ambayo inadaiwa kuwa chini ya udhibiti wa genge la ujambazi. Picha/ Mwangi Muiruri

“Gari lingine la uchukuzi wa umma hata likiwa na idhini ya TLB kufanya biashara katika barabara hii huwa linazimwa na genge hilo. Haijalishi kuwa serikali imekupa idhini ya kufanya biashara hapa. Idhini inayotambulika ni ile ya genge hili,” asema mmoja wa wenyeji wa eneo hilo ambaye anahofia kutajwa.

Anaongeza kuwa wale ambao hukaidi kutii amri za genge hili hujipata wamevamiwa na aidha magari yao kutekwa nyara na kutoroshwa, wahudumu kutandikwa na kujeruhiwa huku wengine wakiuawa.

“Kwa kuwa kwa sasa kuna magari 170 ambayo hutumia barabara hii chini ya mpangilio wa genge hili, ina maana kuwa kwa siku genge hili hujipa pato la Sh34, 000. Hizi ni pesa ambazo hupokezwa maafisa wa kiusalama katika urefu wa barabara hii ili wasiwaandame washirikishi hawa wa kijambazi,” asema.

Kuna wafanyabiashara ambao wamekuwa wakijaribu kuwekeza katika barabara hii lakini huwa wanazimwa na masharti hayo makali ya genge hili.

“Mimi nilikuwa nalenga kuweka magari 50 ya uchukuzi katika barabara hii…Lakini nilihesabiwa gharama ya kuafikia masharti hayo na nikalemewa. Nilishindwa itakuwa namna gani nilipe ushuru kwa serikali kuu nikisaka leseni ya kibiashara, lakini nikitua nyanjani Napata serikali nyingine ambayo sikuichagua kuwa mamlakani ikinidai ushuru,” asema Bw Misheck Njumbi.

Anasema kuwa ako na habari kuwa hata Katibu maalum katika wizara ya usalama wa Ndani Karanja Kibicho amepashwa habari kuhusu genge hili lakini “kutokana na sababu ambazo hatujui, hata yeye ameamua kukaa kimya.”

Ujasiri

Genge hili huwa na ujasiri wa kipekee ambapo katika maandalizi ya makala haya, tulifanikiwa kupata msimamo wa genge hili.

Lilimtaka waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i akome kujihusisha na biashara huru ya matatu

likisema kuwa biashara hiyo huwa na mikakati yake ya kuendeshwa na ambayo serikali haifai kuingilia kwa msingi wa kuithibiti.

Hivi karibuni, Dkt Matiang’i alitoa amri kuwa magenge yote yanayodhibiti uchukuzi wa umma kupitia utozaji wa ada, kuzima biashara huru itambe na pia wanaohangaisha wasafiri katika steji yaondolewe katika sekta hiyo.

“Hatuwezi kuwa na genge la wahuni ambalo kazi yake ni kusimama kwa steji wakitekeleza kila aina ya ukora…Ni serikali pekee ambayo iko na ruhusa ya kutoa leseni za kuhudumu na kusimamia barabara ambazo huwa zimejengwa kwa kutumia ushuru wa umma,” akasema Matiang’i akitoa amri hiyo.

Kwa mujibu wa msemaji wa genge hilo, John Muthungu, kuna maelewano kati ya maafisa wa kiusalama katika barabara hiyo na ambapo hakuna magari mengine yanafaa kukubaliwa yahudumu isipokuwa tu yale yaliyo katika ushirika wa Kigumo Travellers Sacco.

“Kuna maafisa wa polisi ambao wanatumwa na Matiang’i kushika doria katika barabara hii, yakitupa vitisho vya kutuondoa barabarani. Tunataka kumwambia Matiang’i kuwa hii ni biashara huru,” akaambia Taifa Leo katika mtaa wa Heho.

You can share this post!

Straika wa TZ amezewa mzte EPL

MOSES KURIA: Hachoki kujikwaa ulimi kila mara akitafuta...

adminleo