Makala

Mambo kangaja Gachagua, Sakaja wakianza kupigana vijembe tena

Na WINNIE ONYANDO September 13th, 2024 2 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja wameanza tena kushambuliana hadharani huku kila mmoja akitaka kuonyesha ubabe wake.

Wawili hao Septemba 12, 2024 walipeleka mzozo wao katika mtandao wa kijamii wa Facebook kukosoana kuhusu maandamano ya wafanyabiashara kutoka soko maarufu la Marikiti yaliyoshuhudiwa Alhamisi.

Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilisema kuwa itaendelea na mpango wake wa kuwahamisha wafanyabiashara katika soko la Marikiti hadi soko la kisasa lililoko barabara ya Kangundo.

Hii ni baada ya wafanyabiashara hao kukaidi agizo la gavana wa Nairobi la kuwataka wahame katika soko hilo.

Kaimu Katibu wa Kaunti ya Nairobi Godfrey Akumali alisema kuwa uamuzi wa kuwahamisha wafanyabiashara wanaouza viazi, vitunguu na kabichi kwa jumla umepitishwa na hakuna kurudi nyuma.

Kulingana na kaunti hiyo, idadi ya wafanyabiashara na wateja wanaotembelea soko hilo imekuwa ikiongezeka, na kulazimisha wengine kuuzia bidhaa zao kando ya barabara, na hivyo kusababisha msongamano wa magari.

“Wafanyabiashara wanatumia njia ya kubebea mizigo. Hauwezi kuzunguka eneo hilo na hatuwezi kuacha hali hii iendelee. Hatulegei kwa suala hili, lazima wauzaji wa jumla wahamie Soko la Barabara ya Kangundo,” Bw Akumali alisema.

Hata hivyo, Bw Gachagua hakulichukulia jambo hilo kwa furaha.

Alimwandikia Bw Sakaja ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook akimkumbusha kuhusu makubaliano waliyofanya na wafanyabiashara wa Muthurwa wakati wa kampeni za 2022.

“Tuliwaahidi wafanyabiashara kuwa hawatahangaishwa na serikali. Kando na hayo, katiba yetu inaruhusu ushirikishwaji wa umma kabla ya maamuzi muhimu kufanywa,” Gachagua alimwandikia Bw Sakaja kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Bw Gachagua pia alimtaka gavana huyo kukaa chini na viongozi wa soko hilo ili kutafuta suluhu.

“Wafanyabiashara hao walikuamini na ndio maana wakakuchagua. Tafadhali kaa nao chini ili mtafute suluhu,” akaongeza.

Hata hivyo, gavana Sakaja alimjibu naibu rais akimtaka ampigie simu.

“Ndugu yangu mkubwa, una nambari yangu ya simu. Unaweza nipigia simu,” Gavana Sakaja aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Facebook.

Hii sio mara ya kwanza wawili hao kukwaruzana.

Mnamo Mei 2024, wawili hao walishambuliana hadharani kuhusu uongozi wa chama cha United Democratic Alliance.

Bw Sakaja pia amekuwa akimshambulia naibu rais akidai anaingilia mambo yake ya uongozi.

Naye Bw Gachagua amekuwa akimkosoa gavana huyo hadharani hasa kuhusu masuala ya kibiashara jijini Nairobi.