• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
BIASHARA: Gharama ya juu yazima raha ya kilimo cha maua

BIASHARA: Gharama ya juu yazima raha ya kilimo cha maua

NA SAMMY WAWERU

KENYA imejiunga na orodha ya nchi ambazo husafirisha maua ng’ambo kupitia meli za mizigo.

Hatua hiyo inayofasiriwa huenda ikaletea afueni kilimo cha maua, imetokana na kuendelea kupanda kwa gharama ya usafirishaji kwa njia ya ndege.

Aidha, Kenya imekuwa ikitegemea kwa kiasi kikubwa ndege kusafirisha mazao mabichi ya shambani katika masoko ya ng’ambo.

Covid-19 ilipotua nchini 2020, ndege za mizigo zilisimamishwa ili kudhibiti msambao amri ambayo kulingana na mtandao wa wazalishaji na wauzaji iliathiri sekta ya maua.

Mwaka mmoja baadaye, licha ya kuondolewa ndege zote hazikurejea hivyo basi nafasi ya usafirishaji ilipungua na gharama kuongezeka.

“Kabla kukumbwa na virusi vya corona, kilo moja ilikuwa ikisafirishwa kwa Dola 2.4 (Sh287.98 thamani ya Kenya). Kwa sasa, imependa hadi Dola 5.6 (Sh671.94), hivyo basi hatuna budi ila kutafuta njia mbadala kufikisha mazao sokoni,” asema Clement Tulezi, Afisa Mkuu Mtendaji Baraza la Wazalishaji Maua Nchini (KFC).

Uholanzi, Colombia, Israel na Afrika Kusini ni kati ya nchi zinazotumia meli kusafirisha maua.

Tulezi anasema usafirishaji wa bidhaa hiyo kwa njia ya maji ni mojawapo ya mikakati kupunguza gesi hatari ya Kaboni.
Mwaka uliopita, 2021 katika kongamano la COP26 Kenya iliahidi mchango wake kusaidia kuangazia tabianchi.

“Usafirishaji mizigo kupitia bahari utapunguza kuenea kwa Kaboni kwa karibu asilimia 90,” afisa huyo aelezea.

Tabianchi imechangia mabadiliko ya hali ya hewa, na kuathiri sekta ya kilimo kwa kiwango kikubwa.

Siani Flowers, ni miongoni mwa kampuni ambazo zimekumbatia matumizi ya meli kusafirisha maua sokoni, Joshua Kulei, Mkurugenzi akiambia Akilimali ilianza mwaka 2021.

“Tulianza majaribio 2013, na kufikia sasa tumeibuka na mikakati na aina ya maua yanayopaswa kusafirishwa kupitia meli,” Kulei adokeza.

 

Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya Siani Flowers, akihudumia mteja katika maonyesho ya IFTEX, jijini Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Kampuni hiyo husafirisha kontena moja kila wiki, afisa huyo akisema huchukua kati ya siku 24 – 28 mizigo kutua sokoni.
Msongamano na mabadiliko ya ratiba yasiyotabirika, Kulei anataja kama baadhi ya changamoto wanazopitia.

Meli zinazotumika, zimeboreshwa kuwa na vihifadhio baridi ili kudumisha uhalisia wa maua.

Kulingana na takwimu za KFC, Kenya husafirisha makontena 15 – 20 kila wiki baraza hilo likiridhia mchango wa Wizara ya Kilimo, Biashara, Uchukuzi, Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) na ile ya Reli (KRA) kufanikisha jitihada hizo.

Katika Maonyesho ya Kibiashara ya Kimataifa ya Maua (IFTEX), yaliyofanyika jijini Nairobi mwaka huu 2022, KFC na Ubalozi wa Uholanzi Kenya, mkataba wa ushirikiano kufanikisha usafirishaji maua kwa njia ya meli ulitiwa saini.
Mbali na gharama ya juu ya usafirishaji, wakuzaji wanaiomba serikali kutathmini bei ya pembejeo.

“Gharama ya uzalishaji ni ghali mno, ilhali bei ya mazao sokoni haijaimarika. Utendakazi ni mgumu,” alalamika Peter Githua, Meneja wa Mikakati Primarosa, kampuni iliyoko Ol Joro Orok.

Kulingana na data za Taasisi ya Unakili wa Takwimu Nchini (KNBS), 2021 Kenya iliuza ng’ambo tani 210,000 za maua.
Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Finland, Norway, Canada na Urusi ni wanunuzi wakuu wa maua ya Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Mfalme Charles III aahidi kufuata nyayo za mamake

ZARAA: Nafaka mpya zatoa jibu la kudorora kwa mazao

T L