Habari za Kitaifa

Ishara vyama vya UDA na ODM vitafanya harusi kuelekea 2027

Na MOSES NYAMORI September 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VYAMA vya United Democratic Alliance (UDA) na Orange Democratic Movement (ODM) vinavyoongozwa na Rais William Ruto na Raila Odinga mtawalia, vimetangaza uchaguzi wa mashinani Novemba huku kukiwa na mazungumzo ya kuungana katika uchaguzi wa 2027.

Kikao cha Kamati Kuu ya Usimamizi ya ODM kilichoongozwa na Bw Odinga Jumatano kiliagiza Kamati ya Kitaifa ya Uchaguzi (NECC) ya chama hicho kuanza maandalizi ya uchaguzi wa mashinani.

‘NECC inaagizwa kujiandaa kwa uchaguzi wa mashinani ulioahirishwa mnamo Novemba,’ Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna alisema. ODM imefanya mabadiliko katika kamati yake ya uchaguzi na kumteua Bw Hamida Kibwana kuchukua nafasi ya Bi Beatrice Askul, aliyeteuliwa Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda.

Taifa Leo imefahamishwa kuwa chama hicho kinapanga kukamilisha uchaguzi wa mashinani kabla ya kufanya Kongamano la Wajumbe wa Kitaifa kuchagua viongozi wa kitaifa hapo Februari baada ya kujua matokeo ya kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

Anagombea kiti hicho cha Bara ambacho huenda matokeo yake yakaathiri uongozi wa chama.

Tayari Bw Odinga amekabidhi jukumu lake kwa Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o ili azingatie kampeni za AUC kwa ukamilifu.

Mwenyekiti wa NECC Emily Awita alisema kwamba watakutana ili kupanga tarehe na ratiba ya uchaguzi.Naibu kiongozi wa chama cha ODM ambaye pia ni Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema Kamati Kuu ya Usimamizi inayoongozwa na Bw Odinga iliamua kufanya uchaguzi wa mashinani kuanzia vituo vya kupigia kura, hadi wadi na maeneo bunge Novemba.

Alisema tarehe za ngazi ya kaunti na kitaifa zitatangazwa kulingana na matokeo ya awamu ya kwanza.“Mwezi wa Novemba, tutakuwa na uchaguzi kutoka vituo vya kupigia kura hadi ngazi ya maeneo bunge. Kaunti na Kitaifa zitatangazwa baadaye. Hii itakuwa awamu ya kwanza ya uchaguzi kisha chama kitatoa mwelekeo zaidi,” akasema Bw Osotsi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya UDA Anthony Mwaura alisema kuwa bodi hiyo inapanga kuandaa mkutano wiki ijayo ili kupanga tarehe mpya za uchaguzi.

Katika mahojiano ya awali alisema shughuli hiyo itaanza Novemba hadi Desemba. “Tutaanza tena Novemba shule zitakapofungwa. Mpango ni kukamilisha uchaguzi katika maeneo yote kufikia Desemba 15,” Bw Mwuara alisema hivi majuzi.

UDA ilianza shughuli Aprili lakini ikalazimika kuachana nayo baada ya kukamilika katika kaunti mbili pekee za Busia na Homa Bay kati ya tano za awali ambazo ziliratibiwa kushiriki katika awamu ya kwanza. UDA ilikuwa imepanga kukamilisha uchaguzi huo Agosti mwaka huu kabla ya kusitishwa kutokana na maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha wa 2024.

Chama hicho kimeagizwa na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa (ORPP) kukamilisha zoezi hilo ndani ya siku 180 kutoka Agosti.