Michezo

Mwanasoka Capoue ajaribu bahati katika mpira wa vikapu

Na MASHIRIKA September 13th, 2024 1 min read

KIUNGO wa zamani wa Tottenham Hotspur na Watford, Etienne Rene Capoue ameamua kugeukia mpira wa vikapu baada ya kukosa ofa ya kuendelea kutandaza soka.

Capoue alichezea Villarreal kwenye Ligi Kuu ya Uhispania misimu mitatu kabla ya kandarasi yake kukatika Julai 1, 2024.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 36 alisakata jumla ya michuano 148 akiwa Villarreal ikiwemo 40 msimu 2023-2024.

Licha ya kuwa muhimu kwa Villarreal msimu uliopita, klabu hiyo iliamua kutoongeza kandarasi yake.

Amekuwa huru kujiunga na klabu yoyote, lakini hatajapata waajiri wapya katika soka.

Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Get Football News France ambacho kimenukuu tovuti ya michezo ya Relevo mjini Madrid, Capoue anafanya mazoezi na klabu ya mpira wa vikapu ya daraja la nne nchini Uhispania ya CB Jovens L’Eliana, karibu na mji wa Valencia.

“Hata alipata kuichezea katika mechi ya kirafiki hivi majuzi ambayo timu yake ilishinda,” tovuti hiyo ilisema Alhamisi, Septemba 12, 2024.

Capoue, ambaye alichezea timu ya taifa ya Ufaransa ya watu wazima mechi saba kati ya Agosti 2012 na Agosti 2013, alipigwa picha na wachezaji wenzake akiwa mwenye furaha baada ya ushindi huo.

Hata hivyo, Capoue hana leseni ya kuchezea CB Jovens L’Eliana mechi rasmi.

Imetafsiriwa na Geoffrey Anene