Habari za Kitaifa

Kampuni ya Adani yachunguzwa kwa ulanguzi wa pesa

Na ELVIS ONDIEKI, MARY WANGARI September 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KAMPUNI ya Adani Group kutoka India ambayo imezua kizaazaa nchini baada ya kuanza mpango wa kukodi Uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), imemulikwa baada ya fedha zake Sh39.99 bilioni kuzuiliwa nchini Uswizi kwa madai ya ulanguzi wa pesa.

Stakabadhi zilizotolewa mahakamani zinaonyesha kuwa mwanamume ambaye ana uhusiano na benki tano za Uswizi anachunguzwa na Mwanasheria Mkuu wa Uswizi.

Zaidi ya Sh39.99 bilioni zimezuiliwa kutokana na uchunguzi huo.

Mashirika kadhaa yamemhusisha mwanamume huyo na kampuni ya Adani, lakini imekanusha vikali uhusiano wowote naye.

Kulingana na tovuti ya Uswizi, Gotham City, mtu huyo ni mwakilishi wa Adani.

Hata hivyo, Adani amejibu madai hayo, ambayo pia yameungwa na Hindenburg Research ya Amerika.

“Tunakataa na kukana madai yasiyo na msingi yaliyowasilishwa. Adani Group haihusiki katika kesi zozote mahakamani Uswizi, na hakuna akaunti yoyote ya kampuni yetu ambayo imezimwa na mamlaka yoyote,” kampuni hiyo ilisema katika taarifa.

‘Zaidi ya hayo, hata katika amri inayodaiwa, mahakama ya Uswizi haijataja kampuni za kundi letu wala hatujapokea maombi yoyote ya ufafanuzi au taarifa kutoka kwa mamlaka yoyote au shirika la udhibiti,’ iliongeza.

Adani aliwasilisha pendekezo kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya (KAA) mapema mwaka huu kuendesha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) chini ya mkataba wa miaka 30.

Hatua hii imepingwa na mahakamani na ilisababisha wafanyakazi wa uwanja huo kugoma.

Hata hivyo, akiwa mbele ya kamati ya seneti kuhusu uchukuzi, waziri wa uchukuzi Davis Chirchir alisema serikali bado haijatia saini mkataba wowote na kampuni hiyo.