Habari za Kitaifa

Kinachofanya Kampuni ya Joho kushtaki KPA

Na PHILIP MUYANGA September 13th, 2024 1 min read

KAMPUNI  inayohusishwa na familia ya Waziri wa Madini Hassan Joho imeishtaki Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA) na kampuni ya kushughulikia nafaka ya Bulkstream Ltd kwa madai ya kuvuruga biashara yake katika bandari ya Mombasa.

Kampuni ya Portside Freight Terminals Ltd, inadai kuwa KPA na Bulkstream zimeingilia reli ya zamani inayohudumia kituo chake bandarini.

Portside inadai kuwa KPA imetoa ruhusa kwa Bulkstream kubomoa laini tatu za reli ya zamani na kuweka laini moja ya Reli ya Kisasa (SGR) ili kuhudumia Bulkstream pekee kujaza mabehewa yake yenyewe mafuta ya kupikia kuyasafirisha.

Bulkstream Ltd, zamani Grain Bulk Handlers Ltd, inahusishwa na mfanyabiashara wa Mombasa Mohammed Jaffer.

Portside inahoji kuwa athari ya kuinua kuondoa laini hizi ni kwamba itanyimwa vifaa vinavyohitajika kupakia mizigo yake kwenye mabehewa ya reli ya zamani kusafirisha kwa wateja wake.

‘Kwa kifupi, mlalamishi hataweza kupakia shehena yoyote kwa kutumia laini za reli ya zamani kwa usafirishaji,’ stakabadhi za kesi zinasema.

Portside Freight Terminals Ltd inahoji kuwa shughuli za Bulkstream zitasababisha kuzibwa kabisa kwa barabara ya umma inayoelekea kwenye mabohari yake yaliyokodishwa.

Portside pia inasema kuwa KPA ilishindwa kuihusisha na washikadau wengine bandarini kabla ya kufikia uamuzi huo.

‘Katika hali hii, idhini au ruhusa iliyotolewa na KPA kwa Bulkstream Ltd ni batili na haina nguvu yoyote ya kisheria,’ kampuni inasema katika kesi yake.

Kesi hiyo itatajwa Oktoba 2, 2024