Habari za Kitaifa

Gen Z wa Mlima Kenya wasimama na Gachagua


VIONGOZI wa vijana kutoka Mlima Kenya wamewashutumu Wabunge  ambao wamejitenga na Naibu Rais Rigathi Gachagua na kumwidhinisha Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kuwa Msemaji wa eneo hilo.

Wakiongozwa na Mtaalamu wa Usawa wa Jinsia, Dkt Fridah Karani, viongozi hao walishutumu wabunge hao kwa kujihusisha na siasa za migawanyiko badala ya kuangazia maendeleo ya eneo hilo.

Walijitenga na wabunge hao, wakisema hawakushauriwa.’Hakukuwa na ushiriki wa umma na kwa hivyo tunakataa uamuzi wa wabunge,’ alisema Dkt Karani.

Vijana waliapa kupinga hatua yoyote ya kugawanya eneo hilo.’Sisi kama vijana, hatuwezi kusimama na kutazama jinsi siasa za migawanyiko na ajenda za ubinafsi zinatishia umoja wetu, utulivu na maendeleo,’ alisema.

Vijana walisisitiza kuwa ajenda ya mgawanyiko inayoenezwa na wabunge inaonyesha kutojali kabisa usawa wa kijinsia na maendeleo ya eneo lao.

‘Vijana na wanawake wanatengwa katika mijadala muhimu ya kisiasa licha ya kikatiba kuamuru kujumuishwa kwao,’ alisema Dkt Karani.Wabunge 14 kutoka kaunti za Embu, Meru na Tharaka Nithi walitangaza kwamba Prof Kindiki atakuwa msemaji wao wa kuuunganisha eneo hilo na serikali ya Rais William Ruto.

Mnamo Alhamisi, wabunge 48 wa eneo la Mlima Kenya Magharibi pia walijitenga na Bw Gachagua na kumuunga Profesa Kindiki kuwa msemaji wao.

Wabunge walisema wameungana kushawishi maendeleo ya Mlima Kenya.

“Kama viongozi waliochaguliwa kutoka Mlima Kenya, kwa niaba yetu na wakazi waliotuchagua, tumeamua kuwa atakayetuunganisha na serikali kuu ni Profesa Kindiki,” walisema katika taarifa.

Wabunge hao wanaotoka kaunti za Kiambu, Murang’a, Nyeri, Nyandarua, Kirinyaga, Nakuru, Laikipia na Nairobi, walisema Bw Gachagua ameshindwa kuonyesha uongozi bora na kukataa kuungana na Rais kuwaunganisha Wakenya.

“Juhudi zetu za kusaka maendeleo kwa watu wetu zimetatizwa na kukosekana kwa kiongozi ambaye anatuelewa na anayeweza kupeleka maslahi ya watu wetu kwa serikali kuu.

“Hata hivyo, Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango na Mwakilishi wa Wanawake Njeri Maina wamejitenga na wabunge hao wakisema hawakuhusisha maoni ya wakazi wa eneo hilo. Walisisitiza kuwa wabunge hao wamepoteza mwelekeo wa kisiasa, wakionya kuwa huenda wakapoteza viti vyao katika uchaguzi ujao. Wabunge hawa wamekosea na wakazi kutoka eneo hili hawajafurahishwa nao,’ alisema Bw Murango.

Bi Maina alitaja hatua ya wabunge hao kama aibu kwa eneo lao.

‘Naibu Rais ndiye mwanasiasa mkuu kutoka eneo letu lakini cha kusikitisha ni kwamba wabunge wanapigana naye,’ alisema.

Bi Njeri aliapa kuendelea kumuunga mkono Bw Gachagua ambaye alisema ana nia nzuri kwa eneo la Mlima Kenya.

‘Adui zangu wa kisiasa wananiita mfuasi shupavu wa Bw Gachagua. Ni kweli na nitaendelea kumuunga mkono kwa sababu ni kiongozi mzalendo wa Milimani,’ alisema Bi Njeri.