Gachagua akwama na ‘ground’ akitengwa na wabunge
JAPO anaonekana kubanwa na kutengwa na wanasiasa wakuu wa Mlima Kenya, Naibu Rais Rigathi Gachagua angali na nafasi kubwa ya kukuza ushawishi wake katika eneo hili huku wadadisi wakisema ameonyesha sio kiongozi wa kupuuzwa.
Ingawa wanaompiga vita wanaonekana kuongezeka na kuungwa na wenye mamlaka, Bw Gachagua anasisitiza kuwa hatakoma kutetea maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya, ngome yake ya kisiasa ambayo wakosoaji wake wanajenga taswira kwamba inamponyoka.
Bw Gachagua amewapuuza wabunge waliojitenga naye akiwataja kama wasaliti wa wakazi wa Mlima Kenya ambao wanazongwa na matatizo chungu nzima chini ya utawala wa serikali anayohudumia.
“Mimi ninazingatia kuhudumia watu. Puuzeni na kukataa siasa za migawanyiko lakini mtambue vitendo vya kila mmoja na kupima utendekazi wake. Wakenya wanataka viongozi wanaofanya kazi na sio kuzingatia siasa. Wanataka viongozi wafanye kazi,” alisema akiwa Nyeri Ijumaa siku moja baada ya wabunge 48 kutoka ngome yake kujitenga naye.
Kulingana na wadadisi wa kisiasa, hali ya sasa katika Mlima Kenya ni tete na ni wapiga kura watakaoamua hatima ya viongozi wao wa sasa uchaguzini, akiwemo Gachagua.
“Kinachomfanya Gachagua kuwa na imani na nguvu licha ya kutengwa na wabunge wengi wa chama tawala eneo hilo ni kuwa anajisawiri kama mtetezi wa maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya huku wabunge wanaompiga vita wakiunga serikali inayowaumiza kwa sera kandamizi,” asema mchambuzi wa siasa David Kimani.
Anasema kwamba Bw Gachagua amejisawiri kama mtetezi wa wakulima wadogo wa kahawa, chai, makadamia na maziwa na sasa anaweza kuhusisha masaibu ya wakazi na wabunge walioasi ambao wamekuwa wakimlaumu kwa tamaa na kwa kueneza siasa za ukabila
Bw Gachagua amekuwa akiweka wazi kwamba siasa huanza nyumbani na hajuti kutetea maslahi na kupanga siasa za ngome yake kwa lengo la kuwa na nguvu za kujadiliana katika ngazi ya kitaifa.
“Mimi ni mtu anayesikiliza mashinani,” huwa anakumbusha wakosoaji wake kila mara.
Kimani anasema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Bw Gachagua kuibuka na nguvu zaidi kwa kuungwa na wapigakura au hata kuzama zaidi iwapo serikali itamporomosha kwa kutumia bunge kumuondoa mamlakani.
“Ukweli ni kwamba wakazi wa Mlima Kenya wanaumia chini ya serikali ya sasa kuliko zilizotangulia. Hii ndio sababu Gachagua amekuwa akiwataka wabunge kusikiliza jinsi wakazi wanavyosema; kwamba umaarufu wa Kenya Kwanza umefifia katika ngome yao lakini wanaonekana kumpuuza,” akasema.
Mnamo Ijumaa, viongozi wa vijana kutoka maeneo kadhaa ya Mlima Kenya walijitenga na uamuzi wa wabunge walioasi Gachagua wakisema wakazi hawakushauriwa.
Kulingana na mchambuzi wa masuala ya kisiasa Dkt Isaac Gichuki, msimamo wa vijana, ambao ndio wengi eneo la Mlima Kenya sawa na maeneo mengine nchini unaweza kumpiga jeki Bw Gachagua.
“Lakini itategemea mwelekeo wa kisiasa atakaochukua na iwapo hataporomoshwa kisiasa kupitia bunge kwa kuwa dalili zinaonekana kwamba njama imesukwa kumtimua ofisini. Kumbuka kumekuwa na minong’ono ya njama kama hizo na mpangilio wa kisiasa wa sasa chini ya Serikali Jumuishi unaweza kuwa msingi wa kuzifanikisha,” asema Gichuki na kuongeza kuwa Gachagua akiondolewa kwa mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi, itakuwa pigo kwake kisiasa.
Dkt Gichuki anasema matukio ya hivi punde yanaanika wazi uhusiano baridi uliopo kati ya Bw Gachagua na Rais William Ruto kabla ya 2027, huku mpango ukiwa ni kumkweza Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki hatua ambayo anasema ni kugawanya eneo la Mlima Kenya lisizungumze kwa sauti moja katika uchaguzi mkuu ujao.
“Naona hii ikiwa njama mbaya ambayo wanaoisuka hawatafaulu kwa kuwa wakazi wa Mlima Kenya Magharibi ambao ni eneo la Kati la Kenya anakotoka Gachagua ni wengi kuliko wale wa Mlima Kenya Mashariki anakotoka Kindiki. Matatizo ya eneo la Kati pia yanatofautiana kwa kiwango fulani na yale ya Mlima Kenya Mashariki,” asema.
Anasema hata akitimuliwa, anaweza kuongoza uasi mkubwa wa wakazi dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza.
“Itakuwa makosa sana kwa kuwa wakazi watahisi anasulubiwa kwa kutetea maslahi yao,” akasema.
Bw Gachagua amekuwa akiwaonya wabunge wa eneo pana la Mlima Kenya kuwa watajuta katika uchaguzi mkuu wa 2027 wasiposikiza matakwa ya wapiga kura.
“Kuna watu wengi niliowasaidia wakati wa kampeni wakashinda viti wanavyoshikilia leo. Lakini niligundua kuwa ni watu wale wale wanaopanga kuniangusha na kunishambulia,” akasema Bw Gachagua.
“Lakini jambo zuri ni kwamba uongozi wa kiti cha kisiasa unadumu kwa miaka mitano tu. Kwa hiyo watu hao watahitaji msaada wangu 2027. Nitawaunga mkono wale wanaoniunga mkono kwa sasa,” aliongeza.