Wakenya wanaoozea jela Amerika waongezeka
UFICHUZI wa hivi majuzi wa kukamatwa na kufungwa kwa aliyekuwa mgombea urais Mohamed Abduba Dida unaongeza orodha ya raia wa Kenya wanaotumikia kifungo jela nchini Amerika.
Mwalimu huyo wa zamani ambaye aliwania urais mwaka wa 2013 na 2017 kwa sasa anazuiliwa katika gereza la Big Muddy huko Illinois baada ya kupatikana na hatia ya kumnyemelea na kumtisha mkewe waliyetengana.
Wakenya wengine mashuhuri waliozuiliwa nchini Amerika ni wana wawili wa Akasha waliopatikana na hatia ya ulanguzi wa dawa za kulevya na pia kuzuia haki kwa kutoa hongo kwa maafisa wa Kenya katika jitihada za kuepuka kupelekwa Amerika kushtakiwa.
Baktash Akasha alihukumiwa kifungo cha miaka 25 jela mwaka wa 2019 huku Ibrahim Akasha akihukumiwa miaka 23 mnamo 2020.
Ndugu hao wa Akasha walikamatwa Mombasa mnamo Novemba 2014 katika oparesheni iliyoongozwa na Amerika.
Huenda kifungo kirefu zaidi ni cha Brian Musomba Maweu aliyehukumiwa kufungwa jela maisha mwaka 2015 kwa kuhusika na ponografia ya watoto.
Mwaka wa 2014, alichapisha jumbe 121 kwenye tovuti ya Dreamboard–mtandao wa kibinafsi wa wanachama pekee ambao ulikuza unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji wa watoto wadogo.
Kevin Kang’ethe ambaye aligonga vichwa vya habari baada ya kutoroka kituo cha polisi pia sasa anazuiliwa gerezani nchini Amerika baada ya kurejeshwa humo wiki mbili zilizopita.
Anakabiliwa na kesi ya mauaji ya kinyama ya mpenzi wake Margaret Mbitu mwaka jana, 2024. Alitoroka Amerika hadi Kenya baada ya kufanya uhalifu huo lakini maafisa walifuatilia na kumkamata.
Akiwa kizuizini katika kituo cha polisi cha Muthaiga, alitoroka katika hali isiyoeleweka na alikamatwa tena na kurudishwa Amerika kwa ndege ya kibinafsi ya FBI kujibu mashtaka ya mauaji.
Mnamo Septemba 3, 2024 alikana mashtaka na amepangwa kurejea kortini Novemba 5 kesi kusikilizwa. Anazuiliwa bila dhamana.
Ulaghai ukiwemo ulaghai wa mapenzi na ulaghai wa uwekezaji ni baadhi ya uhalifu ambao umepelekea baadhi ya Wakenya kufungwa gerezani Amerika siku za hivi majuzi.
Mnamo Februari Paul Maucha, 59, alipatikana na hatia ya njama ya kuwalaghai watu kwa kuwahadaa walipe pesa kwa kampuni kwa kisingizio kwamba wangepokea faida nzuri za kifedha baadaye.
Mwaka jana, 2023, Florence Mwende Musau alifungwa jela kwa kushiriki katika njama iliyohusisha ulaghai wa mapenzi iliyobuniwa kuwahadaa waathiriwa kutuma pesa kwa akaunti za benki zilizodhibitiwa naye na watu wengine.
Alipatikana na hatia ya kutumia pasipoti ghushi zenye majina tofauti kufungua akaunti za benki ambapo angepokea pesa kutoka kashfa za mapenzi.
Mnamo Mei 2023, mahakama ilimhukumu Abdi Hussein Ahmed kifungo cha miaka minne kwa kula njama ya kusafirisha kiasi kikubwa cha pembe za kifaru na pembe za ndovu za thamani ya mamilioni ya pesa.
Pia, alipatikana na hatia ya kulangua heroin.
Mnamo Januari, Erick Gachuhi Wanjiku, 42, alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kuwashambulia maafisa wa serikali.