Habari za Kitaifa

Rais Ruto akaidi amri yake kuhusu Harambee kwa kutoa mchango wa Sh10 milioni kanisani


RAIS William Ruto amefeli kudhihirisha kwa vitendo hatua yake ya kuzima maafisa wa serikali kushiriki michango ya harambee kama mojawapo ya njia za kupambana na ufisadi.

Alitoa agizo hilo Julai 2024 ili kuzima maandamano ya vijana wa Gen Z waliolalamika kuwa hulka ya viongozi na maafisa wakuu serikalini ya kutoa pesa nyingi katika michango hiyo inaendeleza uovu huo.

Wakati huo, Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, ambaye ni mwandani wa Rais Ruto, alishutumiwa kwa kutoa Sh20 milioni, wakati mmoja, katika harambee, watu wakihoji asili ya pesa hizo.

Lakini Jumapili, Septemba 15, 2024, saa chache baada ya kuwasili nchini kutoka ziara rasmi nchini Ujerumani, Dkt Ruto pamoja na wandani wake walihudhuria Ibada katika Kanisa la Stewards Revival Pentecostal, Nairobi.

Wakati wa ibada hiyo, Rais alijitolea kusaidia katika ujenzi wa jengo jipya katika kanisa hilo baada ya jengo la zamani kubomolewa kutoa nafasi kwa upanuzi wa barabara ya Outering.

Aliahidi kutoa mchango wa Sh10 milioni kufadhili mradi huo licha ya kufahamu fika kuwa wananchi wanachukia mienendo ya viongozi kutoa michango ya aina hiyo, hali iliyolazimisha serikali kuidhibiti.

“Najulikana zaidi kama mshirika mkubwa katika miradi ya ujenzi wa makanisa. Unishirikishe hapo…….. Nimekubaliana na Askofu na nitatoa Sh10 milioni kufadhili ujenzi huu,” Rais Ruto akasema waumini wa kanisa hilo wakishangilia kwa furaha.

Hata hivyo, Rais alijaribu kufafanua kwamba kile alichofanya haikuwa harambee, bali ni “mchango tu”.

“Sharti tujenge kanisa hili kwa neema ya Mungu, tatakuja hapa kuizindua,’ akasema kiongozi wa nchi.

Alipokuwa akitangaza hatua ambazo serikali yake imeweka kuzuia maafisa wakuu na watumishi wa umma kushiriki michango ya harambee, Rais Ruto aliagiza Mwanasheria Mkuu kubuni sheria ya kufanikisha hatua hiyo.

“Mwanasheria Mkuu anaagizwa kuandaa na kuwasilisha sheria ya kufanikisha mpango wa kuweka mikakati yenye uwazi wa kutoa michango kusaidia mipango ya umma na yenye kusaidia wasiojiweza katika jamii,” Dkt Ruto akasema mnamo Julai 29, 2024.

Na mapema mwezi huu wa Septemba, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Aaron Cheruiyot alichapisha mswada unaolenga kudhibiti maafisa wakuu wa serikali na watumishi wa serikali kushiriki harambee.

Kulingana na Mswada huo wa Udhibiti wa Michango ya Umma ya 2024, maafisa hao watahitaji kupata leseni kabla ya kushiriki shughuli zozote za kuchanga fedha.

Aidha, mswada huo unalenga kuweka mwongozo wa kisheria kusimamia uendeshaji wa michango ili kudumisha uwazi na uwajibikaji katika uendeshwaji wa shughuli hizo.

Vile vile, unalenga kukinga Wakenya wasipunjwe kupitia michango feki ya harambee huku ukiweka mwongozo wa kutoa hamasisho kwa umma ili wafanye maamuzi ya busara wanapotoa pesa katika harambee.

Mswada huo pia unapendekeza adhabu kali kwa wale watakaovunja sheria kuhusu shughuli hizo.

“Afisa Mkuu wa serikali au mtumishi wa umma atakayepatikana na hatia ya kuvunja hitaji la kifungu hiki atatozwa faini isiyozidi Sh5 milioni,” inasema kifungu cha 13 cha mswada huo.

Kosa hilo linafananishwa na kosa la uchaguzi ambapo anayepatikana na hatia huzimwa kuwania wadhifa wowote ule.

Kulingana na mswada huo, wanasiasa wanaopania kuwania nyadhifa za umma pia wanazuiwa kushiriki harambee, miaka mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.

Sheria hiyo kielelezo pia inamlazimu aliyefaidi kutokana na michango ya harambee kutaja kiini cha michango hiyo na kuwasilisha maelezo hayo kwa Mamlaka ya Ukusanyaji wa Ushuru Nchini (KRA).

“Mtu atakayetoa michango ya harambee au yule atakayepokea fedha hizo sharti atoe maelezo kwa KRA kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru,” mswada huo unasema.

Raia wa kawaida watakaopatikana na hatia ya kukiuka sheria hii watatozwa faini isiyozidi Sh2 milioni au watupwe gerezani kwa miaka mitatu.

“Mswada huu umetayarishwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa Harambee inatumika kama majukwaa ya kusaidia Wakenya wala sio kuendeleza ufisadi, ubadhirifu wa pesa za umma na maovu mengine ya kiuchumi,” anasema Bw Cheruiyot ambaye ni Seneta wa Kericho.