Habari za Kitaifa

Gen Z aliyemshtaki Mandago hatarini kukamatwa

Na JOSEPH OPENDA September 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA ya Eldoret imeamuru shahidi mkuu katika kesi inayoendelea dhidi ya Seneta wa Kaunti ya Uasin Gishu, Jackson Mandago, kujitokeza mbele yake ikionya kwamba huenda kibali cha kumkamata kikatolewa.

Mercy Tarus amedaiwa kudharau korti baada ya kukaidi agizo lililotolewa Septemba 8, kuhusiana na kesi inayomkabili Seneta Mandago aliyeshtakiwa kwa kufuja Sh1 bilioni zilizotengewa mpango wa kaunti kuhusu elimu ya ng’ambo.

“Mashtaka ya kudharau korti ni uhalifu na kwa hivyo ni sharti ahudhurie yeye binafsi sawa na mashahidi wengine wa upande wa mashtaka,” alisema Hakimu Mkuu Peter Ndege.

Wakili wa washtakiwa, Stephen Kibungei, amemshutumu Bi Tarus ambaye ameomba kusikizwa kimtandao, kwa kuomba mazingira ya kipekee ilhali mashahidi wengine, wakiwemo maafisa wa ngazi za juu kama vile Gavana Jonathan Bii, wamezingatia maagizo ya korti na kujitokeza binafsi.

Aidha, korti imemwongeza muda Mwenyekiti wa Hazina ya Elimu, Kaunti ya Uasin Gishu, Dkt Joel Chelule, aliyekuwa ametoa ushahidi hapo awali.

Dkt Chelule aliomba kuruhusiwa hadi Septemba 27 ili kushughulikia masuala ya kibinafsi, agizo lililoruhusiwa na korti ikisisitiza haja ya ufafanuzi wa kina kuhusu masuala yaliyotajwa na mashahidi wengine.

Kesi hiyo imeratibiwa kurejelewa Septemba 24 na itaendelea kwa siku nne.

Mmoja kati ya mashahidi 202 kutoka upande wa mashtaka alisimulia korti jinsi dada yake alivyomlipia jumla ya Sh1.8 milioni kugharamia masomo, cheti cha usafiri na makazi.

Bw Isaiah Kiplagat, 31, mkazi Eldoret, alieleza korti jinsi ufadhili wa masomo nchini Finland uliotangazwa na Kaunti ya Uasin Gishu 2022, ulivyompa matumaini baada ya kuhangaika bila kazi licha ya kufuzu kutoka Chuo Kikuu cha Moi.

Alituma maombi upesi ambapo alipokea baruameme Julai 19,2022, kutoka kwa Sanna Partamies wa Chuo Kikuu cha Laurea, Finland, aliyemwagiza kuanza masomo mwezi uo huo.

Agosti 31, maafisa wa kaunti, Jairus na Rono walimtembelea Kiplagat na kumwagiza kulipa Sh1.8 milioni kabla ya dada yake Bi Linet Chebet kumsadia kulipa kiasi hicho katika awamu mbili, Sh918,000 na Sh259,000.