Habari za Kitaifa

Wanataka kuiba kura zangu 2027, Kalonzo apiga nduru

Na GEORGE MUNENE September 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amedai kuwa kuna njama ya mapema za  kufanikisha wizi wa kura katika uchaguzi mkuu wa 2027 kwa manufaa ya muungano tawala wa Kenya Kwanza.

Alisisitiza kuwa suala hilo ni lenye uzito mkubwa na uovu kama huo hautaruhusiwa kutokea katika uchaguzi huo.

Bw Musyoka alidai kuwa baadhi ya watu wanapewa zaidi ya kitambulisho kimoja cha kitaifa ili zitumiwe kufanikisha kitendo hicho haramu.

Akiongea katika Kanisa la Kianglikana (ACK) la St Joseph Kandongu, Kaunti ya Kirinyaga, Bw Musyoka alitaja kisa kimoja ambapo mtu mmoja alipewa vitambulisho tisa vya kitaifa.

Hata hivyo, hakufichua jina la mtu huyo au mahala anakotoka.

“Nataka niwaeleza jambo la kushangaza. Mtu mmoja amepewa vitambulisho tisa vya kitaifa katika afisa ya msajili wa wa watu. Mtu kama huyo anaweza kupiga kura mara kadhaa katika vituo mbalimbali bila kugunduliwa,” akasema.

Bw Musyoka ambaye ni kinara mwenza katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya alisema upinzani hautaruhusu uchaguzi mkuu ujao kuvurugwa.

“Wameanza kuweka maandalizi ya kufanikisha wizi wa kura ili upinzani usitwae mamlaka. Hatutakubali matokeo ya uchaguzi yasiyoakisi matakwa ya Wakenya,” akasema.

Bw Musyoka, ambaye ni makamu wa rais wa zamani, aliuliza ni kwa nini maafisa wa idara ya usajili wa watu, Waziri mhusika na maafisa wa usalama waliruhusu mtu mmoja kupewa vitambulisho tisa vya kitaifa.

“Serikali hii imeingiwa na woga na inafahamu kuwa upinzani una nguvu wa kuiondoa mamlakani. Hii ndiyo maana inataka kutumia mbinu bandia kuendelea kusalia mamlakani,” akaeleza.

Kiongozi huyo wa Wiper alimshutumu Rais William Ruto kwa kuanza kampeni za mapema huku akiwaonya viongozi wengine dhidi ya kufanya hivyo.

“Wakati ambapo Ruto alimzindua Raila Odinga kama mgombeaji wa kiti cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) alikuwa akijipigia debe kwa uchaguzi mkuu wa 2027. Yale yote ambayo Ruto anafanya kila mahali ni siasa. Ameanza kampeni za uchaguzi mkuu ujao huku akituambia tuache kampeni za mapema, hatutakubali,” akasema.

Aliapa kuwa upinzani umejitolea kuwakomboa Wakenya kutoka kwa utawala dhalimu wa Kenya Kwanza.

Bw Musyoka alilalamika kuwa uchumi unazorota, ufisadi unaongezeka katika sekta zote za uchumi ilhali serikali ya sasa inajitia hamnazo.

“Hatuwezi kukaa kitako na kutizama nchi hii ikoporomoka. Sharti tulete mabadiliko ya uongozi,” akasema.

Kulingana na Bw Musyoka hatua madhubuti zinafaa kuchukuliwa kuwanusuru maelfu ya Wakenya wanaoteseka kwenye lindi la umasikini na kuimarisha maisha yao.

“Nyakati za enzi ya utawala wa Rais Mwai Kibaki, ushuru ulikuwa unakusanya na kuelekezwa kwa kazi iliyokusudiwa na Wakenya walifurahia maisha bora. Nyakati hizi pesa za walipa kodi zinaporwa na maisha yamevurugika. Upinzani utashirikiana na Wakenya kuleta mabadiliko nchini kwa manufaa ya wote,” akaongeza.

Bw Musyoka aliandamana na Waziri wa zamani wa Ulinzi Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, Gavana wa zamani wa Kiambu Ferdinand Waititu na Mbunge wa Matungulu Stephen Mule.