Kanisa lapinga mpango wa JKIA kusimamiwa na Kampuni ya India
KANISA la Pefa (Pentecostal Evangelistic Fellowship of Africa) nchini limekosoa mpango wa serikali unaolenga kukabidhi usimamizi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta JKIA kwa kampuni ya India ya Adani.
Askofu Mkuu wa Pefa Dkt John Okinda, amesema kanisa lake litasimama dhidi ya mpango wowote ambao unatiliwa shaka na unaofanywa kisiri bila idhini ya Wakenya wengi.
Dkt Okinda amesema hakuna mpango wowote unaoathiri Wakenya unaoweza kufanywa gizani na watu wachache bila kuhusisha umma.
Askofu huyo alimwomba Rais William Ruto kuingilia kati na kuonya kuwa iwapo uwanja huo utatwaliwa na kampuni hiyo, utakuwa na athari mbaya kwa Wakenya.
“Siyo haki kusikia kuna mpango ambao umekuwa ukiendelea kwa miezi kadhaa, unaojulikana tu na watu wachache katika nchi hii. Nikiwa naibu mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Makanisa ya Kenya (NCCK) na rais wa makanisa ya Pefa nchini Kenya, nasimama hapa leo kulaani kwa vikali makubaliano yoyote ambayo yamepangwa bila Wakenya kujua,” Dkt Okinda alisema katika kanisa la Keburanchogu, eneobunge la Mugirango Kusini.
Kasisi huyo alitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapendekezo ya mpango huo, akisema hii ndiyo itakuwa njia ya pekee ya kuwaridhisha Wakenya, ambao tayari wameelezea hasira zao kuhusu suala hilo.
“Tunaomba kwamba kila kitu kisimame na kuangaziwa upya kwa kuridhisha Wakenya. Ni wakati wa kufanya mambo sawa katika nchi hii. Ni wakati wa kutii sheria na kuheshimu watu wa Kenya. Hata wale ambao hawako Nairobi wanahitaji kujua kinachoendelea katika uwanja wetu wa ndege wa kimataifa,” Dkt Okinda alisema.
Alishangaa ni kwa nini serikali zilizopita hazijawahi kufikiria kuuza JKIA na kuongeza kuwa mali yote ya Wakenya lazima ilindwe kwa kila njia.
“Uwanja huu wa ndege wa kimataifa umekuwepo katika serikali nyingi zilizopita. Hautaisha katika utawala mmoja. Baada ya utawala wa sasa, uwanja wetu wa ndege wa kimataifa bado utabaki kuwa mali ya Kenya. Kwa hivyo, Wakenya wana haki ya kuambiwa kuhusu mpango wowote ambao hawauelewi na itabidi waelezwe kinachoendelea,” Askofu Okinda alisema.
Alimkashifu Waziri wa Uchukuzi Davis Chirchir, ambaye alimshutumu kwa kujaribu kuhalalisha kutwaliwa huko kwa miaka 30.
“Usiwe mtetezi wa kitu ambacho wewe mwenyewe hukielewi. Ikiwa hauelewi, hauelewi. Tupe mtazamo unaofaa kuhusu mpango huu wa Adani na chochote kinachohusiana nacho,” Dkt Okinda alisema.