Habari za Kitaifa

Yuko wapi? Taharuki yatanda kuhusu diwani aliyetekwa nyara

Na MARY WANGARI September 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI kutoka eneo la Kaskazini Mashariki wameelezea wasiwasi wao kufuatia kutoweka kwa diwani mmoja eneo hilo huku ongezeko la visa vya watu kutekwa nyara, kukamatwa na kuzuiliwa kiholela vikizidi kuzua taharuki nchini.

Diwani wa Wadi ya Della, Yussuf Hussein, almaarufu kama Tolfiyow, alitekwa nyara siku nne zilizopita na watu wasiojulikana alipokuwa akisafiri kuelekea South C, jijini Nairobi, walisema viongozi hao.

“Utekaji nyara huo ulitekelezwa kijasiri. Alipokuwa akisafiri karibu na Enterprise Road, Hussein alizuiliwa na magari mawili ambayo hayakuwa na nambari za usajili. Waliokuwemo walimteka kimabavu na kuchukua simu ya dereva ili kuzuia mawasiliano ya dharura,” walisema wabunge hao wakihutubia vyombo vya habari Jumanne.

“Kwa bahati, simu yake iliyoanguka ndani ya teksi wakati wa mvutano huo, ilipatikana baadaye na dereva. Dereva aliwajibika kwa kuandikisha ripoti mara moja katika Kituo cha Polisi cha Industrial Area japo hakumfahamu abiria wake.”

Kulingana na wabunge hao, familia ya Bw Hussein tayari imeandikisha taarifa na Idara ya Uchunguzi kuhusu Uhalifu (DCI) katika Kituo cha Polisi cha Makadara katika juhudi za kumsaka diwani.

Licha ya dereva wa teksi kuandikisha ripoti upesi, viongozi hao wamelalamika kwamba uchunguzi umejikokota wakisema hali hiyo,”Inachochea wasiwasi miongoni mwa umma na kuzidisha hofu kuhusu usalama wa Hussein huku kitendo hicho kikiibua taharuki miongoni mwa wanajamii na kuzua maswali kuhusu hali ya usalama katika taifa letu.”

Wakiongozwa na Mbunge wa Eldas, Adan Keynan, wabunge hao wamelalamikia ongezeko la visa vya ukosefu wa usalama eneo hilo wakiapa kuwa hawatapumzika hadi Bw Hussein atakapopatikana.

Wametoa wito kwa DCI na mashirika yote ya usalama kufanya hima kukamilisha uchunguzi wakisema tukio hilo la kumteka nyara afisa wa umma ni tishio kwa taasisi za kidemokrasia nchini.

“Tukio hili la kutatiza limezidi kuibua wasiwasi kuhusu usalama sio tu wa viongozi bali pia raia wa kawaida. Kama mwakilishi aliyechaguliwa anaweza kutekwa nyara waziwazi namna hiyo, inaibua swali: Wakenya wa kawaida wako salama kiasi gani? Tishio hili ni sharti liangaziwe kupitia hatua ya dharura ili kurejesha imani ya umma.”

“Vitendo vya utekaji nyara, kukamatwa na kuzuiliwa kiholela kinyume na sheria sio tu tishio la kibinafsi; ni maovu dhidi ya nchi na tishio la moja kwa moja dhidi ya sheria ambayo ni msingi wa demokrasia yetu na kila hatua inayoidunisha inakiuka mfumo wa jamii yetu,” alisema Bw Keynan.

“Hakuna mtu yeyote, bila kujali hadhi au mamlaka, yuko juu ya sheria. Tumesimama pamoja kupinga jaribio lolote la kudunisha mfumo wa sheria unaolinda uhuru wetu.”