Akili MaliMakala

Unoaji wataalamu katika utandawazi wa Bayoteknolojia

Na SAMMY WAWERU September 18th, 2024 2 min read

HUKU serikali ikiendeleza mikakati kufufua sekta ya kilimo, ukumbatiaji teknolojia za kisasa ndio nguzo kuu ya lengo hilo. 

Hata ingawa imekuwa ikikosolewa pakubwa, mifumo ya Bayoteknolojia ipo katika nafasi murwa kugeuza sekta ya kilimo iwe yenye manufaa anuwai.

Bayoteknolojia ni mfumo unaojumumuisha bunifu za kuongeza jeni, kuboresha mimea na mifugo ili kupata spishi zilizoboreka kusaidia kupambana na kero ya kiangazi, wadudu na magonjwa.

Hali kadhalika, unasaidia kuafikia usalama wa mazao kwa kupunguza matumizi ya kemikali.

Kando na manufaa hayo, unashusha gharama ya uzalishaji wa mazao na chakula.

Picha inayoonyesha mtambo wa kusaga pamba uliovumbuliwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kirinyaga. PICHA|SAMMY WAWERU

Mfumo huu ukiashiria kuzaa matunda hasa katika nchi zilizoukumbatia, Kenya ikiwemo japo unajikokota, umesaidia kuangazia kero ya njaa na uhaba wa chakula.

Kenya, inaruhusu ukuzaji pamba ya kisasa (biotech cotton) na kuiuza, huku mahindi yakiwa yaliidhinishwa 2022 na Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Usalama wa Bidhaa Kibayoteknolojia – National Biosafety Authority (NBA) yakisubiriwa kuwasilishwa kwenye kamati kuyaruhusu kukuzwa.

Mhogo wa kisasa, unaendelea kufanyiwa kaguzi na utafiti.

Taifa likiendelea kukumbatia fani hizi za kisasa na bunifu kuendeleza kilimo, watafiti wanasema Kenya ina nguvukazi ya kutosha ya wataalamu.


Mkulima akionyesha zao la pamba aliyokuza na kuvuna Kaunti ya Embu. PICHA|SAMMY WAWERU

Miongoni mwao ambao nchi inajivunia ni Richard Oduor, Profesa mashuhuri wa Bayolojia ya Molekuli, Uhandisi wa Kijenetiki, Utafiti wa Dawa, na Sayansi ya Uchunguzi wa Kimaabara.

Akiwa mhadhiri na Msajili wa Utafiti, Ubunifu na Ushirikiano wa Kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU), Prof Oduor anasisitiza kwamba kuweka hadharani orodha ya wataalamu wa kibayoteknolojia ya kilimo kutafanikisha nchi kupokea teknolojia za kisasa kuboresha sekta.

“Nimefundisha zaidi ya wataalamu 40 wenye Shahada za Uzamili katika Bayoteknolojia ya Kilimo,” Prof Oduor anafichua, akithibitisha uwezo wa utafiti wa kitaifa.

Richard Oduor, Profesa mashuhuri wa Bayolojia ya Molekuli, Uhandisi wa Kijenetiki, Utafiti wa Dawa, na Sayansi ya Uchunguzi wa Kimaabara aliyenoa vipaji wengi ambao sasa ni wataalamu. PICHA|SAMMY WAWERU

Kulingana na mtaalamu huyu, orodha ya idadi ya watafiti nchini ikiwekwa paruwanja itashangaza wanaodai Kenya haina utoshelevu wa watafiti katika kilimo.

“Tuna wataalamu wa Masuala ya Bayoteknolojia kutoka sekta za kibinafsi na umma, ikiwemo vyuo vikuu,” anaelezea.

Anaongeza, “Listi ikiwekwa wazi, watu watashangaa tunajiweza kuitafiti kama taifa”.

NBA ndiyo taasisi ya kiserikali inayojukumika kuidhinisha matumizi ya teknolojia za kisasa na bunifu.

Prof Oduor anasisitiza kwamba kupiga jeki taasisi za utafiti na zinazoidhinisha teknolojia mpya, ndio nguzo ya ufanisi katika sekta ya kilimo.

Baadhi ya wataalamu wa masuala ya bayoteknolojia kwenye mkutano wa NBA mwaka huu, 2024 wakipata mafunzo ya ziada. PICHA|SAMMY WAWERU

“Tuna uwezo na miundomsingi bora, na endapo serikali itatengea kitengo cha utafiti asilimia mbili pekee ya mpango wake wa ukuaji wa taifa (GDP) tutapiga hatua mbele kuangazia njaa na usalama wa chakula,” anaamini mtaalamu huyo.

Sekta ya kilimo imekuwa ikilalamikia upungufu wa wataalamu, hasa kutokana na kuendelea kustaafu kwa maafisa wakongwe nafasi zao zikikosa kujazwa.

Teknolojia za kisasa na bunifu, zinatajwa kama njia mojawapo kuangazia changamoto zinazozingira kilimo.