Habari za Kitaifa

Wazazi waruhusiwa kuchukua mili ya watoto waliokufa moto shuleni Hillside Endarasha


WANAFUNZI wote walioangamia Septemba 5, 2024 kwenye mkasa wa moto uliotokea katika bweni la shule ya Hillside Endarasha wametambuliwa.

Akizungumza katika Mochari ya Hospitali ya Naromoru, Mwanapatholojia Mkuu wa serikali Dkt Johansen Oduor alisema shughuli hiyo iliyohusu kuwatambua wahasiriwa kupitia kulinganisa DNA imekamilika.

Kulingana na Dkt Oduor, mili yote iliyoteketea kiasi cha kutotambulika ililingana na chembechembe za DNA zilizotolewa kutoka kwa wazazi.

Awali, Dkt Oduor alisema baadhi ya sehemu za mili hiyo hasa miguu ziliteketea kabisa.

Miongoni mwa watoto 21 waliokufa katika mkasa huo wa moto ulioteketeza bweni lililokuwa na wanafunzi 164, wavulana 19 waliteketea kabisa.

“Maabara ya serikali iliweza kulinganisha DNA za wahasiriwa na zile za wazazi. Kwa sasa tunajishughulisha kuhakikisha kuwa familia zimeunganishwa na wapendwa wao,” alisema Dkt Oduor.

Mkuu wa Eneo la Kati wa Shirika la Redcross, Esther Chege, alisema shirika hilo tayari limeanza kuwasiliana na familia zilizoathirika ili kuzifahamisha kuhusu matokeo ya DNA.

Alisema familia za wahasiriwa zitazuru Mochari ya Hospitali ya Naromoru kuanzia Alhamisi, Septemba 19, ambapo zitapitishiwa kipindi cha ushauri nasaha.

“Tunaelewa mafadhaiko ya kihisia yanayowakumba, hivyo kabla ya kuona wapendwa wao, tutawasaidia kutuliza fikra zao na kuwafafanulia wanayopaswa kutarajia,” alieleza