Habari za Kitaifa

Mpango wasukwa kumuongezea Kindiki mamlaka, itakuaje kwa Gachagua?

Na MOSES NYAMORI September 20th, 2024 1 min read

MNAMO 2019 mzozo mkubwa ulipozuka katika utawala wa Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta alimkweza waziri wake wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kwa kumpa majukumu ya ziada ya kusimamia miradi yote ya serikali.

Dkt Matiang’i alikuwa waziri mwenye nguvu, akiwa na mamlaka zaidi kuliko Naibu Rais wa wakati huo William Ruto katika miaka ya mwisho ya muhula wa pili wa Bw Kenyatta.

Aliongoza Kamati ya Kitaifa ya Utekelezaji ya Maendeleo na alikuwa kote nchini akisimamia utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu za Jubilee.

Nia ilikuwa kumtumia Dkt Matiang’i kumzima Dkt Ruto, ambaye alikuwa ametofautiana na mkubwa wake, Rais Uhuru na alionekana kutikisa serikali kutoka ndani.

Ilikuwa pia sehemu ya mpango mkubwa zaidi wa kupanga urithi wa 2022.

Matukio yajirudia

Miaka mitano baadaye, hali kama hiyo inaonekana kuibuka katika utawala wa Kenya Kwanza.

Juhudi za makusudi za kukweza ushawishi wa Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki zimesukwa ndani ya serikali.

Katika siku chache zilizopita,Prof Kindiki amekuwa akiidhinishwa kama msemaji wa eneo la Mlima Kenya na kama kiunganishi cha eneo hilo na Rais kuhusiana na miradi ya maendeleo.

Hatua hiyo inajiri baada ya miezi kadhaa ya madai kuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ana nia ya kutatiza utawala kutoka ndani.

Wabunge, madiwani na zaidi ya wazee 2000 wa Njuri Ncheke kutoka eneo kubwa la Mlima Kenya wameidhinisha Prof Kindiki kama kiongozi wa eneo hilo.

Baadhi ya washirika wa Bw Gachagua waliambia Taifa Leo kwamba Dkt Ruto alikuwa akitumia mbinu iliyotumiwa na mtangulizi wake kumnyanyasa naibu wake.

Mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru almaarufu Mejjadonk, hata hivyo, alipuuzilia mbali mkakati huo akisema hautafaulu.

‘Wanataka kumtumia Kindiki jinsi Uhuru alivyomtumia Matiangi kupigana na naibu wa rais. Hii ni mbinu iliyojaribiwa na utawala wa Jubilee lakini haikufaulu. Itafeli tena,” akasema Bw Gathiru.