Pigo kwa serikali korti ikizima wanafunzi kusajiliwa kwa SHIF
MPANGO wa serikali wa kuwasajili kwa lazima wanafunzi chini ya Hazina ya Afya ya Jamii (SHIF) umepata pigo baada ya Mahakama Kuu kusitisha kwa muda mchakato huo.
Jaji wa Mahakama Kuu, Jairus Ngaah, ameagiza shughuli hiyo ya usajili isimamishwe ili kusubiri uamuzi katika kesi iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria Sheria (LSK).
Kupitia notisi iliyotolewa Agosti 16, Katibu wa Wizara ya Elimu, Belio Kipsang’, aliagiza wasimamizi wa shule za umma kuhakikisha watoto wa shule wanasajiliwa chini ya SHIF.
LSK ilihoji kuwa notisi hiyo ilizua hali ya kukanganyikiwa katika taasisi za elimu na huenda ikawafungia nje watoto wa shule.
“Wakati huo vilevile, hali iliyokuwepo kabla ya agizo au uamuzi uliofutiliwa mbali wa Agosti 16, 2024, itadumishwa kusubiri kusikizwa na uamuzi kuhusu ombi lililowasilishwa au hadi maagizo zaidi ya korti hii. Imeagizwa hivyo,” alisema Jaji Ngaah.
Jaji aliagiza kesi hiyo isikizwe Novemba 8.
Katika kesi hiyo, LSK ilisema Mahakama Kuu ilitangaza Sheria kuhusu Bima ya Afya ya Jamii kuwa kinyume na katiba lakini uamuzi huo ulisitishwa ili kuruhusu serikali na Bunge kufanyia marekebisho baadhi ya vipengee vya Sheria hiyo katika muda wa siku 120.
LSK vilevile ilisema korti iliagiza Bunge kufanya uhamasishaji na ushirikishaji wa umma vya kutosha.