Maoni

Maoni: Kigogo wa Mlima Kenya ni Gachagua mpende msipende

Na DOUGLAS MUTUA September 20th, 2024 3 min read

MCHUKIE ukitaka, lakini kaa ukijua kwamba Geoffrey Rigathi Gachagua, ama ukipenda Riggy G, ndiye kigogo wa siasa za janibu za Mlima Kenya wakati huu.

Wasiompenda watakwambia eti akifungua kinywa hajui kupanga maneno vizuri, ana mazoea ya kujikwaa ulimi, hana mwao na neno diplomasia, na kadhalika.

Hata hivyo, pale Mlimani Gachagua ni ‘mbaya wetu’. Hata akifanya kitu gani, watu wake watamtetea na kufa naye hasa anapopondwa na wanasiasa wasiotoka eneo hilo, hasa washirika wa karibu wa Rais William Ruto.

Nimeandika na kurudia hapa kwamba eneo la Mlima Kenya ni tofauti na mengine yote kote nchini Kenya. Mkondo wa siasa huamuliwa na wananchi, si viongozi.

Wananchi ndio wanaoamua kigogo wao ni nani, si mja wa kujitwika ugogo kwa uchu wa mamlaka tu kama ilivyo kawaida ya maeneo mengine nchini.

Vilevile, kinyume na watu wa maeneo mengine nchini, wenyeji wa Mlima Kenya hawajali kuwa nje ya serikali ilimradi tu wanatetea maslahi yao.

Ni kwa mitaarafu hii ambapo nawacheka mno wanaotishia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Bw Gachagua, wamwondoe mamlakani eti. Ameshikilia cheo hicho kwa dhamana ya wakazi wa eneo hilo, hivyo ukimgusa unawagusa wao.

Kumwondoa Bw Gachagua mamlakani kutampa Dkt Ruto sifa ya dikteta msaliti na hatawahi kusamehewa na eneo hilo. Daima atalaumiwa kwa kuwa chanzo cha njama hiyo kwa sababu kikatiba hana mamlaka ya kumfuta kazi naibu wake.

Hata hatua ya kumwondoa Bw Gachagua ikichukuliwa, kisha ateuliwe naibu rais mwingine kutoka Mlima Kenya, wenyeji hawatamuunga mkono kwa sababu watamchukulkia kuwa msaliti anayetumiwa na maadui zao kumpiga vita kiongozi wao.

Gachagua akiondolewa, Kenya itashuhudia mgawanyiko wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa tena tangu nchi hii iwe huru.

Natumai kwamba msimamizi wake kazini, Dkt Ruto, analifahamu hili fika, au majasusi wa NIS watampa taarifa kamili na za hakika.

Nasema NIS wachukue jukumu hili kwa kuwa nahisi kama kuna watu wanaomdanganya Rais kwamba anaweza kutawala Kenya kwa raha zake bila uungwaji mkono wa Mlima Kenya.

Iliwezekana enzi ya utawala dhalimu wa Daniel Moi, lakini Dkt Ruto si Moi, na hii si Kenya ya miaka ya tisini. Tuna Katiba mpya inayomtaka mshindi wa uchaguzi wa urais apate asilimia 50 ya kura, na angaa kura moja zaidi.

Hicho ni kibarua kigumu mno ambacho sidhani Dkt Ruto anataka kukabiliana nachio kati ya sasa na Uchaguzi Mkuu ujao. Akiwa mwerevu, na binafsi sina shaka na janja zake za kisiasa, atamwacha aliyelala aendelee kulala, lau sivyo alale mwenyewe.

Huu ni ukweli unaojulikana vyema na wanasiasa wote wa Mlima Kenya, hata wanaompinga Bw Gachagua na kumlaumu kwa kile wanachokiita kumkosea heshima kiongozi wa nchi.
Isipokuwa kuzidiwa na kiburi tu, wenyewe wanajua kuwa Dkt Ruto na Bw Gachagua wakikosana hadharani, na utengano utokee, watakaobaki upande wa Dkt Ruto hawatachaguliwa tena ifikapo mwaka 2027.

Naam, hata waliokuwa maarufu namna gani kama vile kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Kikuyu, Bw Kimani Ichung’wa, hawatarejea bungeni. Labda kwa hisani ya mfadhili wao kama wabunge wateule.

Tayari Ichung’wa ameonyeshwa dalili za kutotakikana; hivi majuzi amejaribu kuhutubia umati wa watu katika eneo la Kiambaa wakamkataza kwa kumfokea, akajaribu kushupaza shingo kwa kuwaambia kwamba hatishiwi na yeyote, wakazidisha kelele. Huu ndio mwanzo tu.

Hata mwenzake wa Kiharu, Bw Ndindi Nyoro, ambaye hadi hivi majuzi tu aliaminika kuandaliwa na Dkt Ruto kuchukua pahali pa Bw Gachagua aking’atuliwa, anajua ataliona Bunge paa asipojiunga na upande wa Bw Gachagua. Si ajabu siku hizi amenywea na kufyata.

Ikiwa huamini haya, jiulize iwapo Bw Ichung’wa na Bw Nyoro wanampiku Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwa maguvu ya kisiasa na umaarufu aliokuwa nao kabla ya kujaribisha kuuza kiti-moto Saudia – kuridhiana na Bw Raila Odinga – mnamo mwaka 2018.

Yeyote, awe rais au lofa wa kawaida, akionekana kukinzana na matakwa ya eneo la Mlima Kenya anaweza kuadhibiwa kwa kuchukiwa kama mchawi na kutoungwa mkono katika kila jambo.

Mpaka sasa Bw Kenyatta hajafufuka kisiasa, wala hakuna anayejali anasema nini, akitokea tu anawapa kichefuchefu watu waliomwimbia na kumwombea aingie mamlakani mwaka 2013. Huo ndio uhalisia wa siasa za Mlima Kenya.

Kutokana na msimamo mkali wa eneo hilo dhidi ya watu wanaochukuliwa kuwa wasaliti, tayari picha za wasiomuunga mkono Bw Gachagua zimekusanywa na kuanza kusambazwa mtandaoni.

Maelezo ya picha zenyewe yanatishia kwa sababu yanafanana na tanzia: “Hawa wametuacha ghafla sana; 2027 watakwenda nyumbani.” Sasa usijiulize kwa nini huwasikii sana vilimilimi wengi wa kisiasa kutoka Mlimani.

Rais Ruto anahitaji kila mtu ili kushinda Uchaguzi Mkuu wa 2027. Heri awatulize wanaozozana, aungwe mkono na Bw Gachagua, Bw Odinga na Waziri wa Mambo ya Nje, Bw Musalia Mudavadi, akichaguliwa awaache wazichape mbali na Ikulu wakipania kumrithi.

[email protected]