Makala

Mwalimu mkuu aliyejinyonga Nyamira alisema kifo kitampa furaha

Na WYCLIFFE NYABERI September 21st, 2024 2 min read

POLISI katika eneobunge la Kitutu Masaba kaunti ya Nyamira wanachunguza kifo cha mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Mokwerero, anayesemekana kujitoa uhai Alhamisi asubuhi.
Katika barua ya kutamausha anayodaiwa kuiandika, marehemu Barnabas Nyakundi alisema alikuwa amepoteza tumaini maishani na kwamba ni kifo tu ambacho kingempa faraja.
“Nimechoka. Siwezi kujipigania tena. Kifo kitanipa raha. Nimeshindwa,” ilisoma sehemu ya barua hiyo inayodaiwa kuachwa na Bw Nyakundi.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Manga Benson Makundi alisema marehemu alipatikana akining’inia ndani ya nyumba yake.
 “Tumeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo. Mwili wake ulipatikana ukining’inia ndani ya nyumba yake. Ulihamishwa hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti. Mipango mingine itafuata,” Bw Makumba aliambia Taifa Leo kwa simu.
Kabla ya kuchukua hatua hiyo, marehemu aliwaaga majirani zake na kuwaambia kuwa amepitia madhila mengi ulimwenguni lakini hakueleza ni mateso yapi.
“Ikiwa hamtaniona,  mjue nilishindwa. Nimeteseka ya kutosha,” aliendelea.
Mwalimu huyo alimshukuru mwanamke mmoja aliyemtaja tu kama  Mama Peter kwa kumpa chakula katika siku zake za mwisho duniani.
“Mama Peter ahsante kwa kunipa chakula wiki chache zilizopita. Nimechoka,” alidaiwa kusema.
Mwalimu mwingine alijiua
Zaidi ya miezi mitatu iliyopita, mwalimu mwingine huko Nyamira alikufa kwa kujitoa uhai baada ya kudaiwa kupoteza dau la Sh 50,000 alilokuwa ameweka kwenye mchezo wa kamari ya mitandaoni.
Mwalimu huyo alikuwa wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Nyamira na alipoteza pesa zake katika mchezo wa kamari unaoangazia dhana rahisi lakini ya kuvutia, ambapo wachezaji huweka dau na kutazama kadri kizidishi kinavyoongezeka kadiri muda unavyopita.
Mwalimu huyo alikuwa ameajiriwa shuleni hapo na Bodi ya Wasimamizi. Alifariki katika chumba chake alichopanga. Alikuwa akifundisha Hisabati na Kemia na alikuwa amehudumu shuleni humo kwa miaka minne.
Mnamo Februari 2023, mwalimu mwingine wa Hisabati na Kemia katika Kaunti jirani ya Kisii pia alijiua nyumbani kwake katika kijiji cha Nyosia katika eneo bunge la Nyaribari Chache.
Evans Nyangeso Onchari, ambaye alikuwa mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Senior Chief Musa Nyandusi Kegati, alitaja sababu nne zilizomfanya kujitoa uhai.
Alisema alikuwa akisumbuliwa na pumu ya muda mrefu, shinikizo la damu, saratani ya kibofu cha mkojo na uvimbe wa muda mrefu kiasi kwamba alifikiri kifo ndiyo njia pekee.
Onchari alijinyonga kwenye mti uliokuwa nje ya nyumba yake.