Acheni siasa za majimbo, mbunge akemea wanasiasa wa Mlima Kenya
MBUNGE Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Lamu, Bi Muthoni Marubu, amesuta wanasiasa wanaoendeleza siasa za maeneo au kanda badala ya kupigia debe maendeleo ya nchi.
Akizungumza wakati wa mazishi ya Naibu Gavana wa Lamu, Bw Raphael Munyua Ndung’u, katika eneo la Mpeketoni siku ya Alhamisi, Septemba 19, 2024 Bi Marubu alisema wakati umewadia kwa wanasiasa kuacha siasa zinazoegemea maeneo fulani ya nchi; iwe ni Mlima Kenya au Pwani.
Mbunge huyo alishikilia kuwa viongozi wanaoshabikia siasa hizo za kikanda ni wabinafsi.
Bi Marubu alisema kiongozi stahiki ni yule anayeacha ubinafsi na misimamo yake sugu, na badala yake kuangazia zaidi maendeleo kwa wananchi anaohudumia na taifa nzima.
Alisema endapo viongozi wataendeleza siasa za kanda kama vile Mlima Kenya, basi wakome kusaka usaidizi wa maeneo mengine ya nchi kama vile Pwani iliyo na Bahari Hindi.
“Sioni umuhimu wa siasa za majimbo. Basi nasi Wapwani tutasema watuachie jimbo letu lenye bahari,” akahoji.
“Hata kama hatugusi Mlima na nyinyi basi msiguse Bahari,” akasema Bi Marubu.