Habari za Kitaifa

UDA inavyodandia muafaka wa Raila, Ruto kusaka mrithi wa Waziri Wandayi

Na MOSES NYAMORI September 22nd, 2024 2 min read

UDA sasa inapanga kutumia muafaka kati ya Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga kupenya katika eneo la Nyanza ambalo ni ngome ya kisiasa wa kiongozi huyo wa ODM.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, 2022, chama hicho hakikushinda kiti chochote cha ubunge Luo Nyanza.

Hata hivyo, sasa UDA inapanga kuwasilisha mwaniaji wa ubunge katika eneobunge la Ugunja.

Kiti cha ubunge Ugunja kilisalia wazi baada ya Opiyo Wandayi kuteuliwa Waziri wa Kawi kutokana na muafaka ambao upo kati yake Rais na Raila.

Viongozi wa UDA sasa wanalenga kutumia hilo kupenya Nyanza na tayari baadhi ya viongozi wa ODM wamekumbatia muungano wa Rais na Bw Odinga ukinukia mnamo 2027.

“Kuna matamanio kuwa kutokana na kuwa na serikali jumuishi kuna pendekezo kuwa tuwe na mwaniaji wa UDA Ugunja. Tutashauriana kuhusu hilo na kiongozi wa chama kupata idhini yake,” akasema Katibu wa UDA Hassan Omar.

Kando na Bw Wandayi, Rais Ruto pia aliwateua John Mbadi kuwa waziri wa fedha na waliokuwa manaibu kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogondogo) na Hassan Joho (waziri wa madini).

Maafisa wa UDA pia wanaamini kuwa msukumo ambao Rais ameonyesha wa kumpigia debe Bw Odinga kwenye uenyekiti wa AUC utapunguza uadui ambao wamekuwa wakiupata Nyanza.

Katibu wa UDA Homa Bay Silas Jakakimba hata hivyo, anasema kuwa ushirikiano wa Raila/Ruto haukuwa kwa manufaa ya Nyanza pekee bali kuunganisha nchi.

“Taswira kuu ni kuwa na umoja wa nchi. Hata hivyo, ushirikiano huo unatoa nafasi kwa pande zote mbili kujivumisha,” akasema Bw Jakakimba.

Katibu huyo aliongeza kuwa UDA ilikuwa imeanza kupenya Nyanza kutokana na juhudi za awali ambazo zilitokana na usajili wa wanachama ambao ulikuwa ukiendelea.

“Nyanza kwa sasa imeanza kukumbatia demokrasia na mfumo wa vyama vingi. Hii inatokana na miradi mingi ya maendeleo ambayo Rais ameanzisha Nyanza,” akaongeza Bw Jakakimba.

Mwanasiasa Odoyo Owidi alisema chama tawala sasa kinafanya kazi kwa karibu na ODM na kuna uwezekano mkubwa wawili hao watashirikiana 2027.

“Tuko tayari kujenga muungano 2027 sawa na ulifahamika kama Pentagon. Kwa sasa nia yetu ni kuunganisha ukanda wa Ziwa nyuma ya Rais na nina matumaini kuwa uungwaji huu mkono utadumu,” akasema Bw Owidi.

Mwanasiasa huyo alisema kuwa heri eneo la Nyanza lishirikiane na Rais Ruto badala ya ukanda wa Mlima Kenya ambao umekuwa ukiwasaliti kwenye kila uchaguzi.

“Hata handisheki ya kumuidhinisha Raila ingemfanya tu awe Rais wa mateka iwapo angefaulu mnamo 2022,” akaongeza.

Mapema mwaka huu, chama cha UDA kilianzisha mchakato wa kujiimarisha katika ngome za Raila ambazo ni Nyanza, Magharibi, Kisii na Pwani.