Habari za Kitaifa

Uchaguzi mkuu 2027 bado utaandamwa na kesi tele

Na STEVE OTIENO September 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

UCHAGUZI mkuu wa 2027 bado utagubikwa na kesi chungu nzima jinsi ambavyo imekuwa tangu Katiba 2010 ilipozinduliwa, ikiwa marekebisho kadhaa ya kisheria na kisiasa hayatashughulikiwa kwa wakati ufaao, wataalam wameonya.

Ripoti mpya inayofahamika kama Compendium of 2022 Election Petitions iliyoandaliwa na Tume ya Majaji wa Kimataifa tawi la Kenya, (ICJ-Kenya), imeashiria mianya kadhaa inayotishia kukabili kisheria michakato ya chaguzi zijazo na hata kubatilisha matokeo ya chaguzi.

Masuala tata yaliyotajwa katika ripoti hiyo yanajumuisha hali ya bunge kukosa kutekeleza sheria kuhusu kufadhili kampeni, marekebisho kuhusu haki za sheria za uchaguzi kabla ya chaguzi, kukosa kuainisha sheria kuhusu mamlaka ya mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pamoja na ukosefu wa mwelekeo thabiti kuhusu mpangilio wa ushahidi katika kesi zinazohusu chaguzi.

Tatizo lingine linahusu Kipengee 80 cha Sheria ya Uchaguzi kinachoorodhesha mamlaka anuai ya korti ya uchaguzi bila kuipa mamlaka ya kuangazia upya maamuzi yake hali ambayo imeondoa uwazi kuhusu jinsi korti zinapaswa kuendeshwa zinapotatua malalamishi kuhusu chaguzi.

Ripoti hiyo ilisema, “hakuna ufafanuzi kuhusu sera na majukumu ya uangalizi ya mwenyekiti, mkurugenzi na makamishna wa IEBC.”

Ingawa nyanja ya uchaguzi tayari inakabiliwa na misukosuko, timu hiyo ilisema bado kuna muda wa kurekebisha mianya inayojitokeza.

Mtaalam wa sheria za uchaguzi aliyekusanya na kuhariri nakala hiyo, Luciana Thuo, amependekeza misururu ya mapendekezo za kisera.