Habari za Kitaifa

Kitendawili cha Ikulu kutumia Sh4 bilioni nje ya bajeti bila kufichuliwa

Na BRIAN WASUNA September 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

IKULU na Wizara ya Masuala ya Ndani zilitumia zaidi ya Sh3.8 bilioni nje ya bajeti katika mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 2024, bila matumizi hayo ya ziada kufichuliwa.

Mdhibiti wa Bajeti Margaret Nyakang’o katika ripoti yake ya hivi punde kuhusu matumizi, alifichua kwamba alikataa kuidhinisha karibu nusu ya kiasi cha fedha ambacho Ikulu na Wizara ya Masuala ya Ndani iliomba kutumia nje ya bajeti.

Ikulu iliomba Sh2.858 bilioni kwa ‘usalama wa kitaifa na shughuli za serikali’.

Maombi yote yalitolewa siku hiyo moja – Aprili 9, 2024.

Mdhibiti wa Bajeti aliidhinisha matumizi ya Sh1.242 bilioni.

Wizara ya Masuala ya Ndani iliomba Sh3.165 bilioni, kutokana na kile ilichoita shughuli za usalama za mashirika tofauti.

Ofisi ya Bi Nyakang’o iliidhinisha matumizi ya Sh2.65 bilioni kwa Wizara ya Masuala ya Ndani.

Matumizi nje ya bajeti iliyoidhinishwa yanaruhusiwa chini ya Kifungu cha 223 cha Katiba, kinachoita matumizi ya ziada.

Matumizi kama haya hutengwa kwa hali za dharura zisizotarajiwa kama majanga au pale ambapo matumizi yaliyoidhinishwa awali hayatoshi.

Ni lazima wizara husika iombe idhini ya bunge kwa matumizi angalau miezi miwili baada ya kutoa pesa kwa mara ya kwanza.

Chini ya kifungu hicho cha sheria, serikali ya kitaifa haiwezi kutumia zaidi ya asilimia 10 ya bajeti yake iliyoidhinishwa kwa mwaka huo mahususi wa kifedha.

Sheria inahitaji taasisi inayoomba fedha za ziada katika mwaka wa fedha kupata idhini ya Mdhibiti wa Bajeti.

Katika mwaka wa kifedha wa 2023-24, serikali ya kitaifa ilitumia Sh19.1 bilioni nje ya bajeti.

Matumizi hayo yaliratibiwa katika bajeti za nyongeza za Novemba, 2023 na Juni, 2024.

Taasisi nyingine zilizotumia pesa nje ya bajeti zao zilizoidhinishwa awali ni Wizara ya ICT (Sh221 milioni), Wizara ya Kawi (Sh78 milioni), Wizara ya Kilimo (Sh3.4 bilioni), Wizara ya EAC (Sh1 bilioni), Wizara ya Mazingira (Sh2.02 bilioni), Wizara ya Fedha (Sh3.07 bilioni), Wizara ya Elimu (Sh177.5 milioni), huduma ya Polisi (Sh2 bilioni), Wizara ya Biashara (Sh54.4 milioni), na Wizara ya Ushirika (Sh600 milioni).

Kwa jumla, taasisi za serikali za kitaifa ziliomba Sh30.65 bilioni, kulingana na Ripoti ya Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ambayo inahusu kipindi cha kuanzia Julai 1 2023 hadi Juni 30 2024.

Hata hivyo, ziliidhinishwa kutumia Sh19.1 bilioni.

Kiasi hicho kilifikia asilimia 0.5 ya bajeti ya serikali ya kitaifa, ambayo ilikuwa ndani ya kiwango kinachoruhusiwa.

Ingawa ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti haionyeshi ni usalama upi wa taifa au kazi zipi mahususi Ikulu ilitumia, Rais William Ruto alifanya ziara rasmi nchini Ghana na Guinea Bissau kati ya Aprili 2 na 6, 2024.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed alisisitiza kuwa sehemu ya fedha zilizokusudiwa kwa shughuli za usalama wa kitaifa zilitumika kwa ziara hizo.

“Hali ya usalama wa kitaifa inamaanisha kuwa maelezo mahususi hayawezi kufichuliwa. Usalama wa taifa, ni, usalama wa taifa. Hata Bungeni masuala ya usalama wa taifa huwa yanasikilizwa faraghani,,” Bw Hussein aliambia Taifa Dijitali.

Hata hivyo, msemaji wa Ikulu hakuthibitisha ni kiasi gani cha Sh1.2 bilioni kilitumika kwa masuala ya usalama wa taifa, na ni sehemu gani ilitumika katika shughuli za Serikali.

Pia, Bw Mohamed hakuthibitisha kama safari za Ghana na Guinea-Bissau zilifadhiliwa kwa kutumia pesa hizo.

Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Sh2.65 bilioni yalitokana na oparesheni za mashirika mengi ya usalama, maandalizi ya Siku ya Madaraka 2024, hafla za urais mashinani na fidia ya waathiriwa wa mafuriko jijini Nairobi.

Wizara ya Usalama wa Ndani inayoongozwa na Prof Kithure Kindiki ilituma maombi manane ya kutumia pesa nje ya bajeti kati ya Februari 22 na Mei 27, 2024.