Kimataifa

Jeshi la Israel laangamiza 490 nchini Lebanon likiwinda Hezbollah

Na MASHIRIKA September 24th, 2024 2 min read

HEZBOLLAH, LEBANON

ISRAELI imezidisha vita vyake dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon ikiua takriban watu 490 na kujeruhi wengine zaidi ya 1,650 katika mashambulio makubwa ya anga ambayo yamezua wasiwasi wa kutokea vita vikali.

Hii ni baada ya jeshi la Israeli kushambulia zaidi ya ngome 1,300 za Hezbollah.

Miongoni mwa waliouawa ni watoto 35 na wanawake 58, maafisa wa wizara ya afya ya Lebanon walisema.

Jeshi la Israeli limeonya wakazi wa bonde la Bekaa mashariki mwa Lebanon kukaa mbali na ghala za silala za Hezbollah.

“Tunaendelea kufuatilia maandalizi ya Hezbollah uwanjani ili kuzuia mapema mashambulio yao kwenye eneo la Israeli, na tumezidisha sana mashambulio yetu dhidi ya Hezbollah,” msemaji wa jeshi la Israeli Amirali Daniel Hagari aliwambia waandishi wa habari.

Katika ujumbe uliorekodiwa kwa raia wa Lebanon, waziri mkuu wa Israeli Banjamin Netanyahu amewataka wazingatiea wito wa Israeli wa kuondoka, akisema lazima “wachukulie onyo hilo kuwa sio mzaha.”

Hezbollah, wakati huo huo, ilirusha zaidi ya roketi 200 kaskazini mwa Israeli, kulingana na jeshi.

Hata hivyo, serikali hiyo haikutoa ripoti ni wangapi kati ya waliouawa walikuwa raia au wapiganaji.

Waziri wa Afya Firass Abiad alisema maelfu ya familia pia zimekimbia makazi yao kufuatia masahsbulio hayo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alielezea kusikitishwa kwake na hali inayozidi kuwa mbaya na kusema hataki Lebanon igeuzwe kuwa Gaza.

Naye Mkuu wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema “kuenea kwa mapigano hayo ni hatari sana na kunatia wasiwasi.”

Kwa upande wake, Rais Joe Biden alisema Amerika inajikaza ili kuhakikisha kuwa amani inapatikana katika nchini hiyo huku Pentagon ikitangaza kuwa inatuma “idadi ndogo” ya askari wa ziada kusaidia katika mapigano hayo.

“Kwa kuzingatia kuongezeka kwa mvutano katika Mashariki ya Kati na kwa tahadhari nyingi, tunatuma idadi ndogo ya wanajeshi wa ziada wa Amerika ili kuwaongeza nguvu maafisa wetu ambao tayari wako katika eneo hilo,” msemaji wa Pentagon Maj Jenerali Pat Ryder alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Mapigano hayo yalianza Gaza na sasa yamevuka mpaka na kufika Hezbollah jambo ambalo limesababisha vifo vya maelfu na kufanya familia kadhaa kupoteza makazi yao.

Hezbollah ilisema inaiunga mkono Hamas na haitakoma hadi mapigano ya Gaza yasitishwe.

Siku ya Jumatatu usiku, Israeli ilisema iliua “idadi kubwa” ya wanamgambo wa Hezbollah ilipopiga takriban maeneo 1,600 kusini na mashariki mwa Lebanon.

“Kimsingi, tunalenga miundombinu ya Hezbollah iliyojengwa miaka 20 iliyopita. Hii ni muhimu sana,” Mkuu wa Wafanyakazi wa IDF, Lt Jenerali Herzi Halevi, aliwaambia makamanda eneo la Tel Aviv.