Habari za Kitaifa

Msiguse KICC, Jaji asema akifuta sheria ya ubinafsishaji ya Kenya Kwanza

Na SAM KIPLAGAT September 24th, 2024 1 min read

SERIKALI ya Kenya Kwanza imepata pigo baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali Sheria ya Ubinafsishaji, 2023 na kuitaja kuwa ni kinyume na katiba kwa sababu ilitungwa bila umma kushirikishwa.

Hatua hiyo sasa imeweka breki mpango wa serikali ya Kenya Kwanza ya kutaka kubinafsisha mashirika 11 ya umma.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Chacha Mwita aliamua kuwa Sheria hiyo pia inakiuka jukumu la Bunge la Kitaifa.

Mahakama pia ilisema mpango wa kubinafsisha Jumba la Mikutano la KICC ni kinyume cha sheria kwa vile jengo hilo ni la kipekee ni mnara wa kitaifa.

‘Sheria nzima ya Ubinafsishaji ni kinyume cha sheria na haina maana kwani umma haukushirikishwa,’ alisema jaji.

Kando na hayo, alisema KICC ni turathi ya kitaifa na kuibinafsisha ni kinyume na Kifungu cha 11(2) cha Katiba.

Jaji Mwita alisema KICC ni mnara wa kitaifa unaohitaji kulindwa, na uamuzi wa kuibinafsisha, ni kinyume cha sheria.

Chama cha ODM pia kilipinga ubinafsishaji wa taasisi kumi na moja za serikali kwa sababu ya umuhimu wao wa kimkakati kikisema kuwa mipango ya kuzibinafsisha kama ilivyopendekezwa na utawala wa Kenya Kwanza ilikuwa tishio kwa uhuru wa Kenya.